WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA LAND ROVER FESTIVAL 2024
Leo Jumatatu Oktoba 07, 2024 Kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda amekutana na wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Mkoa huo, kwa lengo la kuwafungamanisha na fursa mbalimbali zilizopo kwenye Tamasha la Land Rover Festival linalotarajiwa kufanyika Oktoba 12-14 ya mwaka huu.
Akizungumza na wafanyabiashara hao waliopo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Utalii, Vyakula na Vinywaji, Mhe. Makonda amewataka kuwa mstari wa mbele kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye Tamasha hilo, akisisitiza kuwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Uongozi wake Mkoani Arusha unakuwa sehemu ya kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Tamasha la Land Rover Festival 2024 linafanyika mwishoni mwa juma hili likiwa na lengo la kusherehekea mafanikio yetu, kubadilishana maarifa na taarifa mbalimbali, kuutangaza utalii wa Arusha na zaidi kuvunja rekodi iliyowekwa na Ujerumani kwenye kitabu cha rekodi cha Guiness, kwakuwa na magari chapa ya Land Rover takribani 632 kwa wakati mmoja mnamo mwaka 2018.