MKURUGENZI MKUU EWURA AWATAKA WAFANYAKAZI KUZINGATIA MKATABA WA HUDUMA KWA MTEJA
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile, amewataka wafanyakazi wa EWURA, kuhudumia wateja wake kwa kuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja.
Ameyasema hayo wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yaliyofanyika katika ofisi za EWURA Makao Makuu, jijini Dodoma.
“Leo ni siku ambayo tunakumbushana ushirikiano uliopo kati ya watoa huduma na wapokea huduma, kwa upande wetu, sisi tunajielekeza zaidi kwenye kuzingatia utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja( Client Service Charter)”. alisema Dkt. Andilile.
Dkt. Andilile ameongeza na kusema, “EWURA hatuna bidhaa tunayozalisha, hivyo kama mtu anataka kutathmini utendaji wetu wa kazi ataangalia zaidi namna ambavyo tunatoa huduma kwa wateja”
Dkt. Andilile alimalizia kwa kuwataka Wafanyakazi wa EWURA kuboresha utendaji kazi na ushirikiano ili kufikia malengo ya taasisi.
Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa EWURA ni maafikiano kati ya EWURA na wateja wake, ambao ni wadau wakuu katika shughuli za udhibiti. Mkataba umeorodhesha wadau wakuu wa EWURA, huduma zitolewazo pia viwango vya ubora wa utoaji huduma ambavyo wateja wanatarajia.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wafanyakazi wa EWURA na baadhi ya wateja waliofika katika ofisi hizo kwaajili ya kupata huduma mbalimbali.