Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua (Riggy G) ametumia Ibada ya Jumapili ya leo kuomba msamaha, ikiwa ni siku moja kabla Wabunge hawajapiga kura kuamua kumwondoa ama abakie kwenye wadhifa huo.

Gachagua akiwa kwenye Ibada katika kanisa moja Jijini Nairobi amesema kama alimkosea yeyote akiwa Naibu Rais wa Kenya, anaomba msamaha kutoka moyoni mwake.

Amemuomba Rais William Ruto, Wabunge waliowasilisha hoja ya kumwondoa madarakani na Wakenya wote kumsamehe kwa makosa yake.

“Nataka kumwambia ndugu yangu, Rais William Ruto, nikiwa katika jitihada zetu za kufanya kazi, kama nilikukosea, tafadhali nisamehe. Kama mkewangu, katika kazi zake za kunisaidia, amekukosea kwa njia yoyote, tafadhali msamehe”. amesema Gachagua

Kwa upande wa Wabunge, Gachagua pia amewaomba msamaha akirejea maneno yake ya kuwatambua wapiga kura wake aliporejea ofisini wa mwaka 2022.

“Huenda mliona kwamba katika kuwashukuru watu wetu na kwa msaada waliompa Rais na mimi, huenda maneno yetu yaliwafanya msijisikie vizuri. Hatukukusudia vibaya, tulikuwa tunawashukuru waliotupigia kura. Kama mnahisi tuliwakosea kwa njia yoyote, tafadhali sameheni”.

Hayo yanajiri wakati hoja ya kumwondoa Gachagua madarakani ikiwa imewasilishwa bungeni kwa kile waliopeleka hoja hiyo wanadai ni mwenendo mbaya na uvunjaji wa katiba.

Wabunge wanamtuhumu Gachagua kwa mambo mbalimbali ikiwa ni.pamoja na kumdharau Rais Ruto na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria tangu aingie madarakani, tuhuma ambazo amezikana akisema ni njama za kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *