WAZIRI CHANA AZINDUA MRADI WA MAJI KILEWANI WA SHILINGI MILIONI 597.6
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameweka jiwe la msingi na kuzindua Mradi wa Maji wa Kilewani wenye gharama ya shilingi milioni 597.6.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kijiji cha Kilewani Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa leo Oktoba 1,2024.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, Mhe. Chana amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inasogeza huduma za maji kwa wananchi na kumtua mama ndoo kichwani.
“Mradi huu umekuja katikati ya Makazi ya wananchi ili msipate changamoto ya kutumia muda mrefu kutafuta maji” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, amewataka wananchi kutunza mradi huo ili ulete manufaa yaliyokusudiwa ya kuwezesha shughuli mbalimbali kama ujasiriamali kufanyika.
Naye, Kaimu Meneja, Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA), Francis Mapunda amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund) na unahudumia wakazi wapatao 3,847.
Ameongeza kuwa mpaka sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 98 na unatoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.