WASICHANA 4,843 WAMERIPOTI KWENYE SHULE MAALUM ZA SAYANSI ZA MIKOA

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema mpaka kufikia leo  wanafunzi wa kike 4,843 wamekwisharipoti  kwenye Shule za Wasichana za Sayansi za Mikoa ambazo zimejengwa kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Shule ya Wasichana ya Sayansi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Mkoa wa Ruvuma iliyojengwa kwenye Halmashauri ya Namtumbo.

Akitoa maelezo kwa Mhe.Rais Samia kwenye uzinduzi huo, Mhe. Mchengerwa amesema kujengwa kwa shule hizo ni maelekezo yake tangu alipoingia madarakani na kwamba zimekamilika na wanafunzi 4,843 wamekwisharipoti na kuanza masomo yao.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa  kwa kidato cha kwanza wanafunzi waliopo ni 1,596, Kidato cha Pili (139), Kidato cha Tano (2,355) pamoja na Kidato cha Sita ni 753.

Ameeleza Sh. Bilioni 108 zimetolewa kwenye mikoa yote kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo ambapo kila Mkoa umepata Sh. Bilioni 4.1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu yote muhimu ya shule na baadhi kuongezewa Sh.Milioni 350 kwa ajili ya ukamilishaji wa bwalo.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Philemon Magesa amesema Sh.Bilioni 4.6  zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 22, mabweni nane, nyumba za walimu tatu (2 in 1), Nyumba ya Mkuu wa shule, Nyumba ya Matron, chumba cha TEHAMA, Maktaba,  bwalo, uzio pamoja na kukamisha kazi ndogondogo.

Ameongeza kuwa shule hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200 na hadi sasa wapo wanafunzi 548 wakiwamo wenye mahitaji maalum.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *