HAKUNA MGONJWA ANAYEBEBWA KWENYE TENGA TUNDURU – MHE. MCHENGERWA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hakuna mgonjwa anayesafirishwa kwa njia ya Pikipiki huku akiwa amewekwz kwenye Tenga kupelekwa kupata huduma za Afya.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa salaam za Wizara kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Tunduru uliofanyika kwenye uwanja wa Ccm wilayani humo tarehe 26.09.2024.
Amesema nimeona taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha mgonjwa akisafirishwa kwenye Pikipiki huku akiwa kwenye Tenga na kueleza kuwa hakuna magari ya kusafirishia wagonjwa na kwa yaliyopo huwagharimu wananchi fedha nyingi kwa ajili ya kupata huduma ya Gari la Wagonjwa.
Napenda kukuthibitishia Mhe. Rais hapa Tunduru hakuna upungufu wa magari ya kubebea wagonjwa na kati ya Magari 535 tuliyoyakabidhi mwaka jana kwa muongozo wako Mhe. Rais hapa Tunduru walipata Magari 4 ya kubebea wagonjwa.
Na Magari hayo yalipekwa kwenye Kituo cha Afya Nakapanya, Matemanga, Mtesi na Kituo cha Afya Nyalasi ambayo yanafanya kazi saa 24 na rufaa zote zinaratibiwa kwa utaratibu maalumu na sio kuchangisha wananchi.
‘Utaratibu unaotumika kusafirisha wagonjwa nikutumia magari ya kubebea wagonjwa (Ambulaces) na kwa kutumia madereva ngazi ya jamii waliosajiliwa wakati wa mfumo wa M-Mama ambapo mfumo huu unahusika na kusafirisha wakina mama wajawazito na watoto wachanga bila malipo yoyote.
Aliongeza kuwa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya madereva wa jamii 20 walioingia mikataba na Serikali; Hivyo taarifa hizi zipuuzwe kwani zinalengo la kuupotosha umma, kuleta taharuki kwa jamii nakuichafua Serikali.