TRUMP ANUSURIKA JARIBIO LINGINE LA MAUAJI

0

Mgombea wa Urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump yupo salama kufuatia jaribio jingine la mauaji lililofanyika Septemba 15, 2024 wakati akicheza gofu kwenye uwanja wake wa West Palm Beach huko Florida.

Vyombo vya usalama nchini Marekani vimethibitisha tukio hilo huku baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vikimtaja mtu aliyefanya jaribio hilo kuwa ni Ryan Wesley Routh (58) kutoka Hawaii.

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo amedai kuwa alimuona mtu huyo akikimbia kutoka kwenye vichaka na kurukia gari lenye rangi nyeusi aina ya Nissan, baada ya maafisa usalama kumfyatulia risasi kadhaa.

Shuhuda huyo alifanikiwa kupiga picha za gari alilopanda mtu huyo na baadae lilizuiliwa katika eneo moja la Kaskazini mwa Florida.

Kufuatia tukio hilo Trump amesena yuko salama na hakuna jambo lolote litakalompunguza kasi katika safari yake ya kuwania kiti cha Urais.

Jaribio hilo limefanyika ikiwa imepita takribani miezi miwili tangu kutokea kwa jaribio la kwanza lililotekelezwa na mtu mwenye silaha ambaye alimshambulia Trump kwa risasi iliyomjeruhi sikioni, wakati wa mkutano huko Pennsylvania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *