POLISI TUNACHUNGUZA KIFO CHA DAKTARI
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wataalamu wengine wa uchunguzi, limesema linachunguza kifo cha Daktari Dismas Dominic maarufu Chami (32), Mkazi wa Ulyankulu aliyekuwa anafanya kazi katika Kituo cha Afya Ulyankulu ambaye amekutwa amefariki dunia huko katika eneo la Kombo Masai Kata ya Malolo Mkoa wa Tabora.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime, imesema “Mwili wake umekutwa ukiwa na dripu yenye dawa ambayo haijafahamika mkononi, Daktari huyu alimuaga Mkuu wake wa kazi na Mke wake September 2,2024 kuwa, anaelekea Tabora kushughulikia akaunti yake ya benki iliyokuwa na changamoto na angelirejea September 3,2024”
“September 4,2024 hakupatikana kupitia mawasiliano yake ya simu, September 10,2024 Daktari Mkuu wa Kituo hicho cha Afya akiambatana na Mke wa Dkt. D Chami walifika katika Kituo cha Polisi na kutoa taarifa ya kutokuonekana kwake toka September 2,2024, tarehe hiyohiyo Dkt. Chami alimtumia ujumbe Mke wake kwa njia ya Whatsapp unaosema “nisamehe sana baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichoanzisha pesa zote zipo akaunti ya CRDB simamia na Watoto wasome kwaheri”
“Baada ya ujumbe huo hakupatikana tena hadi alipopatikana September 13,2024 majira ya saa tatu usiku akiwa amefariki dunia, uchunguzi wa awali umebaini kuwa, alishajaribu kujiua mara mbili”