SERIKALI IMETOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 500 KUINARISHA KITUO AFYA MVUTI – SILAA
Serikali imetoa zaidi ya shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya huduma katika zahanati ya mvuti iliyopo katika Mtaa wa Nkera Kata ya Msongola kwenye Jimbo la Ukonga Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuipandisha hadhi zahanati hiyo na kuwa kituo cha afya.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga Mhe. Jerry Silaa katika ziara yake jimboni humo, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo ambayo yamefikia hatua ya umaliziaji.
“Msongola na Mvuti hii ya sasa, sio ya zamani, kwa miaka mitatu tu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani tumeona mengi, Rais hataki kuona wanawake wa Tanzania wakipata shida za huduma za afya, ndio maana mwezi mei mwaka jana alileta zaidi ya shilingi milioni 500 kujenga majengo ya huduma za uzazi, jengo la upasuaji, maabara na huduma za wagonjwa wa nje (OPD), kwa hiyo hapa haitakuwa zahanati tena, itakuwa kituo cha afya” amesema Mhe. Silaa.
Amewataka wananchi kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo kwenye sekta mbalimbali jimboni humo.
“Tuendelee kushirikiana katika kusimamia maendeleo haya, ndugu zangu tumshukuru sana Rais Samia kwani kwa jimbo letu la Ukonga, ametoa fedha nyingi katika miradi ya afya, na mengineyo, sasa sio lazima yeye aje kuzungumza nanyi, mkiniona mimi nimekuja hapa maana yake namwakilisha yeye katika kuwaletea maendeleo ” amesema Mhe. Silaa