JUMUIYA YA UMOJA WA ULAYA WATOA TAMKO

0

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, pamoja na Mabalozi wa Uingereza, Canada, Norway, na Uswisi, wameeleza kusikitishwa kwao na matukio ya hivi karibuni ya vitendo vya ukatili, kupotea kwa watu, na vifo vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu nchini Tanzania.

Katika tamko la pamoja lililotolewa na mabalozi hao siku ya Jumanne tarehe 10 Septemba 2024, wametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo, huku wakitoa pole kwa familia zote zilizoathirika.

Katika tamko hilo, mabalozi hao wametoa wito kwa serikali ya Tanzania kuhakikisha usalama wa raia na upinzani, wakisihi utekelezaji wa mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha haki za msingi na uhuru wa kujieleza.

“Tunaunga mkono ahadi ya Rais Samia Suluhu kupitia mpango wake wa ‘4R’, wa kuhakikisha haki za msingi za wananchi na uhuru wa kujieleza unalindwa.” wameeleza katika tamko lao.

Pia wamemhimiza Rais kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo vya ukatili na kuhakikisha kuna uwajibikaji.

Mabalozi hao wameonesha wasiwasi mkubwa kwamba matukio hayo yanatishia misingi ya demokrasia na haki za wananchi, huku wakisisitiza kuungana na Watanzania katika kulinda amani na utulivu wa nchi.

“Matukio haya yanaweza kuathiri sana uhusiano wa kimataifa wa Tanzania, hasa kama haki haitatendeka. Tupo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu.” wameeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *