UTEKELEZAJI KAMPENI YA CHANJO: MIFUGO MILIONI 6 YACHANJWA NDANI YA WIKI 2

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo imefanyika kwa mafanikio ambapo takribani Mifugo Milioni 6 imechanjwa na kutambuliwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo Julai 02,2025 hadi sasa.
Mhe. Dkt. Kijaji asema hayo wakati wa tukio la kuanza kwa kampeni hiyo mkoani Dodoma lililofanyika Wilaya ya Bahi Julai 15, 2025 ambapo ametoa shukrani kwa wafugaji kote nchini kwa namna walivyojitokeza tangu kuanza kwa zoezi hilo ambapo amewaomba kuendelea kufanya hivyo kwa kipindi chote cha miezi miwili ya utekelezaji wake.


“Mhe. Rais amedhamiria kutekeleza kampeni hii kwa wafugaji wote bila kumuacha hata mmoja na ndio maana amewawezesha maafisa Mifugo kwenye kata zote pikipiki na mafuta yake ili waweze kuwafikia wafugaji wote hivyo sitegemei kuona mtaalam yoyote wa Mifugo akiwa ofisini wakati wa utekelezaji wa kampeni hii” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo kwenye tukio hilo ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Nyingo amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo una manufaa kwa Watanzania wote ambapo wengi watanufaika kupitia mzunguko wa fedha zitakazotokana na kuuzwa kwa Mifugo hiyo kwenye masoko ya nje.