SERIKALI YATOA MILIONI 669 KUJENGA KITUO CHA AFYA MADILU, MKUU WA WILAYA NA MBUNGE WATOA NENO


Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Madilu, wilayani Ludewa, mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo ya pembezoni.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Ilininda na Madilu, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mheshimiwa Olivanus Thomas, alieleza kuwa fedha hizo zimetolewa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta ya afya. Alifafanua kuwa mradi huo mpya hautahusisha kumalizia majengo ya zamani bali utaanza na ujenzi wa majengo mapya ya kisasa.

“Nawaomba wananchi wa Madilu kuupokea mradi huu kwa mikono miwili. Huu ni mradi wenu, na serikali imesikia kilio chenu. Nawapongeza kwa hatua mliyofikia kwa kujitolea kuanza ujenzi kwa nguvu zenu wenyewe. Mmeonesha moyo wa uzalendo na dhamira ya kweli ya maendeleo,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Ndugu Castor Kibasa, wakuu wa idara mbalimbali pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Mheshimiwa Joseph Kamonga.
Kwa upande wake, Mbunge Kamonga alieleza kuwa amekuwa mstari wa mbele kupigania upatikanaji wa kituo cha afya katika kata ya Madilu kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo ambayo yamekuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma bora za afya.
“Kabla ya uamuzi huu, wananchi walikuwa wakisafiri umbali mrefu hadi katika vituo vya Mundindi na Lugarawa kupata huduma za matibabu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio chetu na kutuletea fedha hizi ambazo tayari zimewasili,” alisema Mbunge Kamonga.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Dkt. Twilumba Lihweuli, alisema kuwa kituo hicho kitakuwa cha kisasa na kitaambatana na majengo muhimu ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lenye vyumba vya madaktari, maabara, mapokezi na sehemu za mapumziko ya muda mfupi, jengo la upasuaji, jengo la kuchomea taka, kufuria pamoja na miundombinu mingine muhimu.
Kwa upande wao, wananchi akiwemo Diwani mstaafu wa kata ya Madilu, Eugin Mlwilo, na wakazi wa kijiji hicho Lawi Mnyanga, Upendo Mgeni na Deokara Mlwilo walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kusikiliza wananchi na kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo. Pia walimpongeza Mbunge wao kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wa Ludewa wanapata maendeleo.
Ujenzi wa kituo hicho cha afya unatarajiwa kuleta afueni kubwa kwa wakazi wa kata ya Madilu na vijiji jirani ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za afya kwa muda mrefu.