NHC YABORESHA MAKAO YA WAPANGAJI KASKAZINI, MKURUGENZI MKUU AVUTIWA NA UBORA WA MATENGENEZO KILIMANJARO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa kutembelea miradi mbalimbali ya matengenezo ya nyumba na ujenzi unaoendeshwa na Shirika hilo kwa kasi na ubora wa hali ya juu.
Akiwa mkoani Kilimanjaro, Bw. Abdallah ametembelea na kukagua nyumba zilizofanyiwa ukarabati mkubwa katika maeneo ya Uru Estate na eneo la kati mjini Moshi. Nyumba hizo ni miongoni mwa mali za Shirika zinazofanyiwa matengenezo kupitia mpango maalum wa kitaifa wa kuboresha miundombinu ya makazi katika miliki za NHC nchi nzima.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu amewapongeza mafundi na timu ya NHC mkoani Kilimanjaro kwa kazi nzuri, na kwa kuhakikisha nyumba hizo zinarejea katika hali ya kuvutia na salama kwa matumizi ya muda mrefu.
Aidha, amewasihi wapangaji kutunza nyumba hizo kama sehemu ya kuwajibika, ili ziwahudumie kwa kipindi kirefu na kuendeleza hadhi ya maeneo wanayoishi.

“Matengenezo haya yanafanyika kwa ajili yenu – wamiliki wa sasa na wapangaji wa kesho. Tunajenga mazingira bora ya kuishi, kufanya kazi na kuendesha biashara. Tunapoboresha nyumba, tunaboresha maisha,” alisisitiza Bw. Abdallah.
Mpango wa Matengenezo ya Kitaifa wa NHC ni jitihada ya Shirika kuboresha mali zake ili ziwe za kisasa, zenye thamani kubwa, na zinazokidhi mahitaji ya wapangaji wa leo na kesho.
NHC inaendelea kujivunia kazi inayofanyika mikoa mbalimbali nchini – na sasa ni zamu ya Kanda ya Kaskazini kung’aa!
