WIZARA YA MAJI YAKABIDHI KISIMA CHA MAJI BUIGIRI

0
IMG-20250618-WA0009

Wizara ya Maji imezindua na kukabidhi kisima chenye uwezo wa kutoa maji lita 12,000 na kuhudumia zaidi ya wakazi 120 wanaoishi katika eneo la Shule maalum ya Msingi ya Buigiri wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.

Kazi ya uchimbaji wa kisima hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji chini ya ardhi unaotekelezwa na Taasisi inayosimamia rasilimali za maji chini ya ardhi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC-GMI) katika nchi 16 za SADC.

Akizungumuza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday, amesema mradi huo umefadhiliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kupata fedha kutoka Benki ya Dunia(WB).

Amesema hapa nchini mradi huo umetekelezwa katika kata ya Nzuguni na Buigiri jijini Dodoma na kwamba lengo la kuutekeleza ni kuendeleza juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha makao makuu ya nchi yanapata maji safi na salama yenye kujitosheleza.

Ameishukuru SADC GMI na WB na wadau wote waliowezesha itekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa na manufaa makubwa huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kugusa maisha ya watu na kutimiza lengo la upatikanaji wa huduma bora ikiwemo maji safi na salama kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *