HUDUMA ZA NHC KIVUTIO WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2025

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma wameendelea kujitokeza kwa wingi katika banda la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo kwenye viwanja vya Chinangali Park, wakionesha shauku kubwa ya kufahamu taratibu za kupata nyumba bora na za kisasa zinazojengwa na shirika hilo.
NHC ni miongoni mwa taasisi za umma zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayoendelea jijini hapa, ambapo maafisa wa shirika hilo wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma na miradi ya NHC.

Maafisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bi. Mariam Chisumo na Bw. Abbu Mwangu, wamesema kuwa wananchi wamekuwa na hamasa kubwa ya kutaka kuelewa namna ya kununua au kupanga nyumba zinazojengwa na NHC katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan Dodoma.
“Wananchi wengi wanapenda kupata makazi bora. Tunafurahi kuwaelimisha kuhusu taratibu za upangaji, ununuzi, pamoja na miradi inayotekelezwa hapa Dodoma,” amesema Bw. Mwangu.
Kwa mujibu wa maafisa hao, NHC ina jukumu la msingi la kujenga nyumba za makazi na majengo ya biashara kwa ajili ya kupangisha au kuuza, sambamba na kusimamia miliki hizo pamoja na kukusanya kodi ya pango. Aidha, shirika hilo pia linahusika na usimamizi wa miradi ya ukandarasi, upangaji wa majengo, kutoa huduma za ushauri wa kitaalam, pamoja na kuzalisha na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya ujenzi.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yamefunguliwa rasmi leo, Juni 17, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ambaye amepongeza taasisi za serikali kwa kushiriki kwa wingi mwaka huu, huku akiwataka watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa.
Maadhimisho haya yalizinduliwa rasmi Juni 16 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 23 Juni, 2025.