KATIBU MKUU WA UTUMISHI AIPONGEZA MAANDALIZI YA BANDA LA NCC

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI), Bw. Juma S. Mkomi, ametembelea banda la Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma leo na kukagua maandalizi yake.
Akiwa na viongozi wengine kutoka katika ofisi hiyo ya Rais (UTUMISHI) miongoni mwao akiwa ni Mkurugenzi Benard Makhanda na Mkurugenzi Msaidizi Jafari Maganga, Katibu Mkuu amepongeza maandalizi ya banda hilo na kusikiliza maelezo kuhusu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na NCC.
Katika maelezo hayo yaliyotolewa na Afisa Habari na Uhusiano Mkuu wa NCC, Bi. Namsembaeli Mduma, Katibu Mkuu alielezwa baadhi ya majukumu hayo kuwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu, uratibu wa usuluhishi wa migogoro inayohusu sekta ya ujenzi na uandaaji wa fahirisi ya bei ya vifaa vya ujenzi.
Majukumu mengine ni kuratibu na kufanya utafiti, ukaguzi wa kiufundi wa miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa nchini, kutoa mafunzo yakuwajengea uwezo wadau wa sekta ya ujenzi, wakiwemo wahandisi, wakadiriaji majenzi, wabunifu majengo na wengine kutoka katika sekta mbalimbali.
Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza Juni 16, mwaka huu, itazinduliwa rasmi kesho na kuhitimishwa Juni 23, mwaka huu.