LINDI JUMBO KUZALISHA TANI 40,000 ZA MADINI KINYWE KWA MWAKA

●Utafiti umebaini uwepo wa tani milioni 5.5 za madini kinywe.
●Uzalishaji utadumu kwa miaka 24.
●Zaidi ya Wafanyakazi 290 wameajiriwa.
Ruangwa, Lindi
Imeelezwa kwamba kampuni ya Lindi Jumbo inayojishughulisha na uchimbaji wa madini kinywe mkoani Lindi imetabanaisha kuwa ina uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 40,000 za madini hayo kwa mwaka ikiwa pamoja na uchakataji.
Hayo yamesemwa leo Juni 13, 2025 na Paul Shauri ambaye ni Meneja Uhusiano wa kampuni ya Lindi Jumbo inayoshiriki katika maonesho ya madini na fursa za uwekezaji yanayoendelea wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Shauri amesema kuwa, mgodi wa Lindi Jumbo unazalisha aina mbalimbali za madini kinywe ikiwemo Super Jumbo, Jumbo large na Jumbo fine ambazo zinapangiliwa kulingana na ukubwa wa punji za madini yanayozalishwa.


Akielezea kuhusu muda utakaodumu katika uzalishaji wa madini hayo , Shauri ameeleza kuwa, kulingana na utafiti uliofanyika umebaini uwepo wa hifadhi ya takribani tani milioni 5.5 ambazo zitachimbwa kwa muda wa miaka 24.
Kwa upande wa sekta ya ajira ndani ya mgodi huo, Shauri amesema mpaka sasa kampuni imeajiri wafanyakazi 290 , ambapo asilimia 43 ya wafanyakazi hao wanatoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi na asilimia 52 ni wafanyakazi wanatoka nje ya vijiji vya mgodi huku asilimia 5 wanatoka nje ya nchi.

Kuhusu soko la madini, Shauri amesema, kwasasa soko kuu la madini yanayozalishwa na Lindi Jumbo lipo nchini India, hata hivyo kampuni inaendelea na jitihada mbalimbali za kutachakata madini hayo kulingana na uhitaji wa masoko katika nchi mbalimbali kama vile China na Ujerumani.
Kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia madini kinywe yanatumika kutengeneza betrii za magari hususan kwenye magari yanayotumia mafuta, hutumika kwenye mikanda ya breki za magari, hutumika kulainisha sehemu za mitambo yenye joto kali.
Pamoja na matumizi mengine, madini kinywe pia hutumika kutengenezea vikombe (Crucible) kwenye viwanda vya chuma lakini pia hutumika kutengeneza paneli za umeme jua hii ni
kutokana na sifa yake ya kuhimili joto kali.


