TIMU YA MAMA SAMIA LEGAL AID YAKUTANA NA UONGOZI WA MKOA WA DAR ES SALAAM


Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 11 Juni, 2025 imekutana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila kwa lengo la kuanza maandalizi ya Uzinduzi na utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani humo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni miongoni mwa agenda kubwa ya Mhe. Rais ya kuhakikisha migogoro inatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

“Tunapotatua migogoro tunaleta amani. Katika Mkoa wa Dar es Salaam wapo Wananchi wenye Matatizo mbalimbali ya Kisheria ambayo yanahitaji ufumbuzi. Niwaombe Viongozi tuelekeze wananchi wenye matatizo wajitokeze na wapate taarifa ili wafike wapate tiba ya matatizo waliyonayo.”Alisema Mkuu wa Mkoa
Aidha, Chalamila amesisitiza timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kupata taarifa za kina kwa Wananchi watakaowasilisha migogoro yao kwani kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya Wananchi kuanza upya migogoro pindi wanapokutana na watoa huduma wapya hata kama wanajua sio Haki yao.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara Ester Msambazi amesema kuwa Wizara kwa sasa imeifikia mikoa 30 kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ambapo Dar es Salaam itazindua na kuhitimisha awamu ya kwanza ya Kampeni na hivyo kufanya idadi ya Mikoa kuwa 31.

Msambazi amesema kuwa, Wizara imejipanga katika kuhakikisha Wananchi wanahudumiwa kwa kupatiwa elimu ya Kisheria na Msaada wa Kisheria kupitia utatuzi wa migogoro mbalimbali.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Juni 16, 2025 katika viwanja vya Maturubai Mbagala na Mgeni rasmi wa halfa hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).