NHC YATEKELEZA MABADILIKO MAKUBWA, YATOA GAWIO LA BIL. 5.5 KWA SERIKALI

Katika hafla ya kihistoria iliyofanyika leo katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepata heshima ya kutajwa miongoni mwa taasisi tatu bora zilizofanya maboresho ya haraka na ya kuigwa katika utoaji wa gawio kwa Serikali. Hii ni baada ya Shirika hilo kuongeza gawio lake kutoka Shilingi Bilioni 1 mwaka uliopita hadi kufikia Shilingi Bilioni 5.5 kwa mwaka huu wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Ndg. Nehemia Kyando Mchechu, alilitaja Shirika la Nyumba la Taifa kama mfano bora wa taasisi zilizopokea kwa vitendo maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza tija, ufanisi na uzalishaji wa mapato kwa taasisi za umma.

“Kundi la tatu ni la mashirika yaliyoongeza mchango wake kwa kasi zaidi… la kwanza katika kundi hili ni Shirika la Nyumba la Taifa, ambao wametoka katika kiwango cha shilingi bilioni 1 hadi bilioni 5.5. Wameonesha mabadiliko makubwa na ya kuigwa,” alisema Mchechu.
Tuzo ya mfano wa hundi ya gawio hilo ilikabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Dkt. Sophia Kongela, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ndg. Hamad Abdallah.
Shirika la Nyumba la Taifa limekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi mkubwa, likijikita katika ujenzi wa miradi ya kimkakati inayochochea uchumi wa taifa, kuongeza ajira, na kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na ya bei nafuu.

Hafla hiyo ya upokeaji wa gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, ambayo mwaka huu yalifikia takriban 256, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Taasisi, Wenyeviti wa Bodi pamoja na Wakurugenzi Wakuu.
Katika salamu zake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwapongeza viongozi na taasisi zote zilizowasilisha gawio, akisisitiza kuwa fedha hizo zitachangia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma za kijamii kwa wananchi.