MBOGWE YAWA MFANO SEKTA YA MADINI, YAFIKIA 70% YA MAKUSANYO

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameupongeza Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe kwa kazi nzuri inayofanya ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali madini ambapo kufikia mwaka 2024, Sekta ya Madini imefanikiwa kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa.
Dkt. Kiruswa alitoa pongezi hizo akiwa katika ziara maalamu Wilayani Mbogwe ambapo alipokea taarifa ya maendeleo ya Sekta ya Madini katika mkoa wa kimadini wa Mbogwe iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed.

Dkt. Kiruswa aliwasisitiza watendaji wa Ofisi ya Madini Mbogwe kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo katika mnyororo wa thamani madini ili kuendelea kuifungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine kiuchumi.
Awali , Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed alieleza kwamba, kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mkoa wa kimadini wa Mbogwe zimepelekea kufikia asilimia 70 ya makusanyo ya maduhuli kwa kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Juni 2025.
Akielezea kuhusu mipango endelevu iliyowekwa ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kutoa mchango mkubwa kwa wilaya na taifa kwa ujumla, Sakina alibainisha kuwa, mpaka sasa zaidi ya vitalu 5000 vya madini vimetolewa kwa wananchi kwa lengo la kushirikisha wananchi katika kuendeleza uchimbaji ili kuongeza tija ya uchumi kwa ngazi ya wilaya na taifa.


Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe Mhandisi Jeremiah Hango alitabaibisha mikakati mbalimbali iliyowekwa na mkoa ikiwa pamoja na kufuatilia kwa ukaribu migodi iliyosimama kwa muda mrefu ili kubaini changamoto husika na kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali.
Mkakati mwingine ni kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu miradi ya ujenzi wa miundombinu ya serikali na sekta binafsi ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa na wakandarasi ili kukusanya maduhuli yatokanayo na madini ujenzi.
Pia, kuendelea kutoa huduma za haraka pamoja na ushauri wa kitaalam wadau wote waliowekeza katika miradi ya kimkakati ya uchenjuaji ya (CIP)na (CIL) kwa mujibu wa Sheria ya Madini na kanuni zake.

