MUHAS YAPATA VIFAA VYA KISASA KUBORESHA MAFUNZO NA HUDUMA YA KINYWA NA MENO

0
IMG-20250604-WA0106

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kupitia Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno, kimepokea msaada wa viti viwili vya kisasa vya kutolea huduma ya kinywa na meno kutoka Tanzania Cantonese Chamber of Commerce kwa kushirikiana na kampuni ya Foshan DYM Medical kutoka China.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea msaada huo iliyofanyika leo Juni 4, 2025 Mkuu wa Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno – MUHAS, Dkt. Ferdinand Machibya, amesema  kuwa viti hivyo vimebuniwa kwa teknolojia ya hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kamera maalum inayomwezesha mgonjwa kuona moja kwa moja tatizo lililopo kwenye kinywa chake.

“Teknolojia hii si tu kwamba inaboresha utoaji wa huduma, bali pia inaongeza ufanisi wa kufundishia. Viti hivi vina uwezo wa kutumika kuwahudumia wagonjwa wengi kwa haraka, lakini pia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wengi kwa wakati mmoja,” amesema Dkt. Machibya.

Dkt. Machibya ameeleza  kuwa Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno ya MUHAS ndiyo taasisi pekee kubwa nchini inayotoa mafunzo ya kitaalamu kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza hadi ya uzamivu.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kukuza na kuboresha huduma za afya ya kinywa nchini.

Aidha, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kutoa rasilimali muhimu zinazowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, na kuongeza kuwa msaada huo utachangia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kutokana na uwezo wa viti hivyo kufundishia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

“Kwa niaba ya MUHAS na Shule ya Afya ya Kinywa na Meno, napenda kuwashukuru sana Tanzania Cantonese Chamber of Commerce pamoja na Foshan DYM Medical kwa mchango wao mkubwa katika kuendeleza elimu na huduma za afya ya kinywa na meno nchini,” amesema Dkt. Machibya.

Kwa upande wake, Meneja wa kampuni ya Foshan DYM Medical – Instrument Co. Ltd Bi. Bonnie Hong, , amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya jitihada za kampuni yao katika kusaidia utoaji wa elimu na huduma bora za afya ya kinywa  hasa kwa wataalamu kwa afya.

“Tunaamini kuwa kwa kusaidia taasisi kama MUHAS, tunachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha lengo la kuwa na jamii yenye afya bora ya kinywa,” amesema Bi. Hong.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *