WAZIRI DKT. KIJAJI AWAASA WANANCHI KUACHA KUTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI

0
4

Watanzania wamekumbushwa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki kwani athari zake ni kubwa kwa afya ya binadamu na viumbe hai pamoja na mazingira kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Viwanda na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipotembelea mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 2, 2025 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mhe. Dkt. Kijaji alisema kuwa mifuko ya plastiki isipodhibitiwa ikitupwa ovyo na kuingia kwenye vyanzo vya maji vikiwemo bahari na maziwa ina athari kubwa kwa samaki na mazalia yake.

“Sote tutatambue mifuko hii si salama kwa maisha yetu pamoja na mifugo na samaki, kwa mfano inapoingia baharini samaki wenyewe wakimeza mifuko hii ya plastiki haiwezi kumeng’enywa na mwisho wake hufa,” alisisitiza.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Kijaji alitoa wito kwa wafugaji wote nchini kuzingatia ufugaji ulio endelevu usioweza kuharibu mazingira ikiwemo kukata miti ovyo kwa ajili ya maja ni ya malisho.

Alibainisha kuwa malishio yanatoka kwenye mazingira na kwamba wafugaji wanahitaji malisho ya kudumu na endelevu ndio maana Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na mbegu ambazo zimeshapata ithibati kwa ajili ya miti ya malisho.

Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inahamasisha kila mfugaji kuwa na eneo lake kwa ajili malisho na kuepuka kulisha mifugo kwa kuhamahama kwani kunachangia uharibifu wa mazingira

Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Kijaji alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya kazi nzuri ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu urejelezaji na utenganishaji wa taka na kuzitambua kuwa zinaweza kuwa ni mali kwa kutengenezea bidhaa na kulinda mazingira.

Kutokana na hatua hiyo alihimiza wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira kuanzia nyumbani na hata maeneo ya kazi sanjari na kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani.

Akitoa taarifa kwenye banda la Ofisi ya Makamu wa Rais Mratibu wa
Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaoratibiwa na Ofisi hiyo Dkt. Damas Mapunda alisema unawezesha wananchi kufanya shughuli zisizoharibu mazingira.

Dkt. Mapunda alisema mradi huo pia unawawezesha wananchi kujipatia kipato ikiwemo kufuga nyuki katika misitu ambayo ni njia mojawapo ya kulinda mazingira.

Alisema katika maonesho hayo wamekusanya wajasiriamali wanaowezeshwa na mradi ambao wanaonesha bidhaa wanazozalisha huku wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu namna mradi huo unavyowakomboa.

Dkt. Mapunda alitaja Halmashauri saba zinanufaika na mradi huo zikiwemo Iringa Vijijini (Iringa), Wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu “Mazingira yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na Maisha. 

Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani kitakuwa Juni 5, 2025 katika Kiutuo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *