SHINYANGA KUNUFAIKA NA MIRADI YA REA, WAUZIWA KWA RUZUKU MITUNGI 13000

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeitambulisha kampuni ya Lake Gas Limited ambayo imepewa jukumu la kusambaza mitungi ya gesi 13,020 itakayouzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 katika Mkoa wa Shinyanga.
Hayo yamebainishwa leo Juni 2, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Bi. Annet Ndyanabo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji mitungi ya gesi yenye ujazo wa kilo sita mkoani humo.
Mha. Ndyanabo amesema kuwa mitungi ya gesi 13,020 itakayosambazwa mkoani Shinyanga ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambao una lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi kufikia asilimia 80 ifikapo 2034.

“Utekelezaji wa mradi huu unaenda sambamba na malengo ya Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia (2024-2034) ambao unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya watanzania wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034,” Amesema Mha. Ndyanabo.
Ameongeza kuwa, lengo la mradi ni kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia kwa kuwawezesha wananchi wengi kumudu gharama za bidhaa za nishati safi ili kutunza mazingira.

“

Mradi huu utapunguza umaskini kwa kuwapa muda zaidi wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi pindi wanapotumia mitungi ya gesi kama njia mbadala ya kupikia badala ya kuni na mkaa,” Ameongeza Mha. Ndyanabo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni ameipongeza REA kwa kuja na mradi huo na kuiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hiyo muhimu.

Naye, Mratibu wa nishati safi kutoka kampuni ya Lake Gas Limited, Bw. Ramadhan Siasa amesema watatekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili kuchochea matumizi ya nishati hiyo.
Gharama ya Mradi huo ni shilingi 272,769,000 na wilaya zitakazonufaika ni pamoja na Wilaya ya Shinyanga, Kishapu, Ushetu na Msalala na kila wilaya itapata mitungi 3,255.
