BUNGE LAPITISHA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 164.1 SEKTA YA ARDHI

0
502752189_10078898835501264_6952597124155701386_n.heic

Bunge limepitisha na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kiasi cha shilingi 164,146,052,000/= ili kuendelea kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini.

Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 jijini Dodoma leo tarehe 29 Mei 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, wizara hiyo imejipanga kuwahudumia watanzania katika sekta ya ardhi ili kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, Wizara ya Ardhi inakusudia kuanzisha Kamisheni ya Ardhi ambayo itaweka mfumo mmoja wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika ngazi zote hatua aliyoieleza kuwa, itasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta.

“Tumechelewa sana kuwa na Kamisheni ya Ardhi, tumechelewa sana kuhakikisha nchi yetu imepangwa na kupimwa. Kamisheni itasaidia uwajibikaji katika mamlaka zote katika shughuli za sekta ya ardhi zinatekelezwa katika ngazi ya Wizara, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa” amesema Waziri Ndejembi.

Aidha, Waziri Ndejembi ameweka wazi kuwa, ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, Wizara ya Ardhi imependekeza kuwepo Sheria ya Milki itakayoanzisha Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Milki (RERA).

Mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kuunda mfumo madhubuti wa usimamizi wa sekta ya milki, kuratibu na kutunza taarifa wadau na soko la milki, kusimamia tija na ufanisi wa wataalam wa sekta pamoja na kudhibiti uhalifu wa utakatishaji fedha haramu.

“Natoa wito kwa wadau wote wa sekta ya milki kuhakikisha wanasajiliwa na kutambuliwa na Serikali ili kuimarisha ushirikiano na ukuaji endelevu wa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi” amesema Waziri Ndejembi.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa jimbo la Mtera mkoa wa Dodoma Mhe. Livinstone Lusinde ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kuwahudumia watanzania kwa kutenda haki ili kuacha alama kwa watu kupata haki zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *