GURUDUMU LA MAMA LAZINDULIWA RASMI DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewataka Maafisa Usafirishaji Dodoma maarufu kama bodaboda kuacha kutembea na tairi zilizoisha ‘kipara’ kwenye pikipiki zao ambazo husababisha ajali zinazopelekea vifo na vilema vya maisha.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo wakati akizindua rasmi kampeni ya Gurudumu la Mama @GurudumuLaMama ,eneo la Machinga Complex Jijini Dodoma yenye lengo la kupunguza ajali za Bodaboda Nchini kwa kuwawezesha Madereva Bodaboda kupata tairi mpya kwa mkopo nafuu wa kulipa taratibu taratibu.

‘Nimefurahi kuona bodaboda kila siku wanaongezeka hapa Dodoma, Bahati nzuri niliwauliza kwamba mnapata abiria wakasema tunapata, Hizi ni juhudi za Rais wetu Samia kwenye kuboresha Mkoa wetu wa Dodoma kuwa na watu wengi, Sababu vikao na mikutano mikubwa inafanyika hapa, Sijaja na takwimu kamili lakini ajali nyingi zinasababishwa pia na uchakavu wa matairi’ – Mhe. Senyamule.
Aidha Mhe Senyamule ameongeza kwa kusema tatizo la Matairi kwa ajili ya Madereva bodaboda tayari limepata suluhisho ‘Tatizo la matairi tayari tumepata mtu wa kutatua huyu anaitwa Road master, Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuileta hili Gurudumu la Mama Dodoma, Sababu tunaona ajali nyingi zinasababisha Vijana kupoteza maisha na suala la ulemavu wa kudumu’ Mhe. Senyamule.

Nae Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde amewataka Madereva hao bodaboda kuwa waaminifu kwenye matairi wanayokopeshwa na kuwataka kuwa na mshikamano na ushirikiano kupitia vikundi walivyovianzisha ili waweze kufanikiwa zaidi.
Mratibu Mkuu wa Gurudumu la Mama @GurudumuLaMama ,Thuwein Makamba amesema kampeni hii kwa Mkoa wa Dodoma imelenga kushirikisha zaidi ya Madereva bodaboda 1,000 katika awamu ya kwanza na itaenea nchi nzima wakishirikisha Vyama vya Waendesha Bodabodakatika kila Mkoa, ‘Tumeanza na Dodoma, Mtaona Kwa mara ya kwanza nchini vijana wa bodaboda wanapata fursa ya kupata matairi mapya kwa mpango rahisi wa kulipia kidogo kidogo bila dhamana, mkopo kutoka benki pia hakuna masharti magumu’ – Thuwein Makamba.

Makamba ameongeza kwa kusema ‘Haya yote yanafanyika chini ya mwamvuli wa Dira ya Mama Samia ya kujenga uchumi jumuishi unaowagusawatu wa kawaida moja kwa moja, Kampeni hii ni mpango wa kitaifa unaolenga kupunguzaajali zinazotokana na matairi chakavu na kuwawezeshavijana kuongeza kipato kupitia usafirishaji salama’ – Thuwein Makamba.
Gurudumu la Mama ni kampeni inayoongozwa na kampuni ya utengenezaji wa matairi iitwayo ROADMASTER ambayo wamejizatiti kwenye Uhai na Maendeleo kwa Wapambanaji wa Barabarani. Kupitia Uongozi wa Rais Samia umeifanya sekta binafsi iwe daraja kati ya Sera za Mama na maisha halisi ya vijana wa mtaani kwa kufungua milango ambayo leo hii, tairi limepatikana kwa kijana, kesho itakuwa ni Bima. Keshokutwa mkopo wa pikipiki yenyewe.


