BASHUNGWA ATOA SIFA NA ZAWADI KWA ASKARI NA WATUMISHI, ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA KUJITUMA

0
IMG-20250528-WA0032

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amesema Serikali inatambua na kuthamini utendaji kazi wa Wakuu wa Vyombo vya Usalama, maafisa, askari na watumishi raia kwa kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na uwajibikaji wa hali ya juu katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na utulivu, amani na usalama.

Bashungwa ameeleza hayo katika hafla ya kutoa sifa na zawadi kwa askari, wanamichezo na wafanyakazi bora wa vyombo vya usalama na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2025, iliyofanyika tarehe 27 Mei 2025, jijini Dodoma.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza askari na watumishi raia kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mafanikio ya utulivu, amani na usalama tuliyonayo ndani ya taifa letu yanatokana na juhudi za kila mmoja wenu,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amewataka viongozi wa wizara, wakuu wa vitengo, wakuu wa vyombo, pamoja na wakuu wa mashirika na taasisi zilizo chini ya wizara kuendelea na utaratibu wa kuthamini na kutambua mchango wa watumishi sehemu za kazi.

Aidha, Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini mchango wa watumishi walio katika sekta ya usalama, ambapo ameendelea kuongeza bajeti inayowezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.

Bashungwa amewasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kulinda tunu ya amani, kwani ulinzi na usalama wa nchi unaanza na mwananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amesema wizara imetoa sifa na zawadi kwa askari 20, pamoja na vyeti kwa wafanyakazi bora na wanamichezo 117 ambao walitambuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku ya Mei Mosi na kupewa zawadi.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Vita Kawawa, ameipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuwatunuku zawadi na sifa askari na watumishi, kwani kitendo hicho kinawatia moyo na kuongeza ari kwa watumishi kufanya kazi kwa bidii na kujituma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *