LESOTHO WAVUTIWA NA REA

Serikali ya Lesotho imevutiwa na namna ambavyo Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijiji (REA) imepiga hatua katika suala zima la usambazaji wa nishati safi maeneo ya vijijini.
Hayo yamebainishwa Mei 27, 2025 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Nchini Lesotho, Tankiso Phapano akiwa ameambata na ujumbe wa wataalam katika Sekta ya Nishati nchini humo.

“Tumefuatilia kwa karibu katika suala la Nishati, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua na zilizofanikiwa kwa upana wake na tupo hapa leo hii kubadilishana uzoefu na kujifunza siri hii ya mafanikio iliyowafikisha hapa,” alisema Phapano.
Alipongeza jitihada binafsi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala la uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wake.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa nishati maeneo ya vijijini nchini Lesotho, Meneja Kitengo cha Umeme Vijijini (REU), Leloko Mokhutsoane alisema kwa sasa nchini humo, suala la usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini linasimamiwa na kitengo kilicho ndani ya Shirika la Umeme la Lethoso (LEC).


Alisema kutokana na kusuasua kwa ufanisi wa kitengo hicho pamoja na mahitaji ya nishati safi ya kupikia hisusan maeneo ya vijijini nchi hiyo inakwenda kuanzisha Wakala wa Nishati Vijijini.
“Hiki ni kitengo tu tena kinahusika na umeme peke yake na sio nishati kwa upana wake; kwa sasa nasi tunataka kuwa na Wakala wa Nishati Vijijini kama ilivyo hapa Tanzania ili suala la nishati safi nalo liingie na tusijifungie kwenye umeme tu,” alisema Mokhutsoane.
Akizungumzia uendeshaji wa shughuli za Wakala hapa nchini kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu alieleza historia ya wakala hadi kufika sasa.
Mhandisi Olotu aliueleza ujumbe huo namna ambavyo REA ilianzishwa, mafanikio iliyopata hadi sasa sambamba na mipango inayoendelea kutekelezwa.
“REA Tanzania ilianzishwa rasmi mwaka 2007 na wakati huo vijiji 506 pekee vilikuwa vimefikiwa na umeme kati ya vijiji 12,318,” alifafanua Mha. Olotu.


Aidha, Mha. Olotu alieleza kuwa Tanzania Bara ina jumla ya vitongoji 64,359 ambapo hadi sasa vitongoji 33,657 sawa na asilimia 52.3 tayari vimeshafikishiwa umeme.
Aliongeza kuwa, upelekaji wa umeme katika vitongoji 30,702 unaendelea ambapo vitongoji 7,736 vipo katika miradi inayoendelea na vitongoji 9,000 REA ipo katika hatua ya ununuzi wa wakandarasi ambao inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025.
Aliueleza ujumbe huo kuwa hadi kufikia mwaka huu 2025 vijiji vyote 12,318 vimefikishiwa nishati ya umeme na sasa kazi inayoendelea ni kufikisha umeme katika vitongoji.
Ujumbe huo ulipata wasaa wa kujadiliana na wataalam kutoka REA masuala mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za Wakala.