DKT. KIJAJI AWATANGAZIA VITA WANAOTOROSHA MIFUGO KWENYE MINADA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wafanyabiashara ya mifugo nchini hususani wanaosafirisha mifugo hiyo kwenda nje ya nchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi kwani katika uongozi wake hatakubali kuona utoroshaji wa mifugo kwenye minada unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
Mhe. Kijaji amesema hayo leo Mei 27, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Mnada wa Kileo uliopo Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro ambapo amesema kumekuwepo na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaaminifu ambao hufanya biashara kinyume na taratibu, na hutumika na wafanyabiashara wa nchi jirani kununua na kutorosha mifugo kwa siri kwa kutumia vipenyo visivyo rasmi kwenda nchi jirani
“Wakati mwingine wafanyabiashara kutoka nchi jirani huingia na kwenda moja kwa moja katika minada ya awali kwa kuwatumia wenyeji kununua mifugo hiyo na kuisafirisha kinyume na taratibu, wanaofanya hivi wanahujumu mapato ya Serikali pia wanadidimiza ustawi wa Sekta ya mifugo na Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi yao na mimi waziri wa mifugo na uvuvi hilo sitalikubali” amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Kuhusu Mnada huo wa Kileo aliouzindua Mhe. Dkt. Kijaji amesema Ujenzi wa wake umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 208. 9 utasaidia kutoa fursa za kimkakati katika kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi ambapo Mnada huu una uwezo wa kupokea ng’ombe 500 na mbuzi na kondoo 3000 kwa mara moja, na kusisitiza utunzaji wa miundombinu yake ili iweze kuwanufaisha wafugaji na wafanyabishara ya mifugo.
Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji alioufanya katika Sekta ya Mifugo na kuhakikisha wafugaji nchini wanapata masoko ya mifugo yao kwa kujenga pamoja na kukarabati minada ya mifugo 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 17.5, ambayo imewezesha ongezeko la biashara ya mifugo nchini kutoka shilingi trilioni 1.5 mwaka 2021/22 hadi trilioni 3.7 mwaka 2024/25.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte amesema Mnada wa Mpakani wa Kileo ni moja ya Mnada wa kimkakati kati ya Minada 10 iliyopo mpakani mwa nchi, ukiwemo Minada ya Songea, Kagera, Tanga, Arusha na maeneo mengine yaliopo mpakani mwa nchi.
Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa amesema wao kama Mkoa huo utazishirikisha Halmashauri zote kuhakikisha Miundombinu ya Mnada wa Mpakani Kileo inalindwa na kutunzwa ili iweze kutoa huduma na kutoa tija kwa wafugaji na wafanyabiashara wote wa Mifugo.