NHC YATUNUKIWA CHETI CHA SHUKRANI KWA KUDHAMINI TUZO ZA MUZIKI

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetunukiwa cheti cha shukrani kwa mchango wake mkubwa kama mdhamini wa Tuzo za Muziki wa Injili Tanzania, tukio ambalo limefanyika tarehe 23 Mei 2025 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Cheti hicho kimetolewa na waandaaji wa tuzo hizo kama ishara ya kutambua na kuthamini ushiriki wa NHC katika kukuza muziki wa Injili nchini.
Tuzo hizo zimewaleta pamoja wasanii 350 wa muziki wa Injili kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, ambapo walishindanishwa katika makundi 18 tofauti. Kila kundi lililenga kutambua vipaji na kazi bora katika tasnia ya muziki wa Injili, ikiwa ni pamoja na wale walioleta mageuzi chanya na wale wanaosaidia kukuza vipaji vya wasanii chipukizi.

Akizindua rasmi tuzo hizo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Winfred Mahundi, aliwapongeza wasanii kwa ubunifu wao, uzingatiaji wa maadili, na mchango wao katika kulea jamii kiroho pamoja na kuongeza pato la taifa kupitia sanaa.
Mchakato wa kuwachagua washindi ulisimamiwa kwa umakini na uwazi na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mchango katika tasnia ya muziki wa Injili unatambuliwa na kuthaminiwa.
Miongoni mwa washindi wa tuzo hizo ni mwanamuziki mahiri Rose Mhando, ambaye ametunukiwa tuzo maalum kwa mchango wake mkubwa katika kukuza muziki wa Injili nchini. Tuzo hizo zilifanyika chini ya kaulimbiu “Muabuduni Bwana kwa Furaha”.
Ushiriki wa NHC katika tukio hili ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo kuunga mkono shughuli za kijamii, kiroho na kiutamaduni zinazolenga kuijenga jamii yenye maadili na mshikamano.