TANZANIA YAZIDI KUJIIMARISHA UHIFADHI WA URITHI WA UTAMADUNI NA HISTORIA


Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha juhudi za kuhifadhi urithi wa historia na utamaduni kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho kina mpango wa kuanzisha makumbusho ya kudumu.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi mahususi za kuthamini, kuendeleza na kuhifadhi mila, desturi na historia ya taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maonesho ya utamaduni wa makabila mbalimbali ya Tanzania, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Dkt. Christowaja Ntandu, amesema kuwa kuanzishwa kwa makumbusho ya kudumu UDOM kutachangia katika kukuza tafiti za kitaalamu, kutoa mafunzo ya stadi za ujasiriamali, pamoja na kuwapa vijana fursa za kujiajiri na kujiendeleza kitaaluma.
“Tutaangalia namna bora ya kusaidia juhudi za kuanzishwa kwa makumbusho ya kudumu, kushirikiana katika tafiti, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kusaidia vijana wanaotaka kuanzisha miradi ya kiutamaduni na utalii kama njia mpya ya kukuza utalii wa kiutamaduni,” amesema Dkt. Ntandu.

Aidha, Dkt. Ntandu ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya urithi wa historia na utamaduni, hasa kwa kuwawezesha vijana kupata elimu itakayowawezesha kutambua fursa zilizopo ndani ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amesema kuwa chuo hicho tayari kina mikusanyo na vielelezo vya kitamaduni, hasa kutoka jamii ya Wagogo, kama hatua ya awali kuelekea kuanzishwa kwa makumbusho rasmi chuoni hapo.

“Niwahakikishie kuwa chuo chetu kitaendelea kuwekeza katika kukuza vipaji, stadi za uongozi, maadili ya Kitanzania na ujenzi wa taifa kupitia elimu jumuishi yenye mwelekeo wa maendeleo. Tutahakikisha kila mwanafunzi anayehitimu hapa anatoka akiwa na maarifa, ujuzi na moyo wa kujitegemea,” amesema Prof. Lokina.
Maonesho hayo yaliyopewa kaulimbiu “Utamaduni Wetu ni Moyo wa Taifa Tuuenzi” yalipambwa na maonyesho ya utamaduni wa Kabila la Wahaya, ngoma na mavazi ya asili ya makabila ya Kigogo, Kisukuma, Kimasai, Kihehe, Kihaya na kutoka Zanzibar.


