WANANCHI NJOMBE WAFURAHIA HUDUMA YA KUUNGANISHIWA UMEME KUPITIA REA


Wananchi wa vitongoji na vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Njombe wameonesha kufurahia huduma za usambazaji na uunganishaji umeme vijijini kupitia REA.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma kuhusu miradi ya kusambaza umeme vijijini, wananchi wa mkoa wa Njombe wamesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya umeme kwa gharama nafuu ya Shilingi 27,000/- tu.
Pia, wananchi hao wamefurahia huduma ya kifaa cha Umeme-tayari (Ready-board) ambacho kinamuwezesha mwanachi kuunganishiwa umeme bila ya kufanya wiring katika nyumba. Aidha, wameipongeza Serikali kupitia REA kwa huduma hiyo kwa kuwa inawapunguzia gharama za wiring.

Mkazi wa Kijiji cha Ihanga. Christina Mlowe, amesema ” Mimi mjane mmeniwekea huu umeme wa kupunguza gharama za wiring, sikutegemea haya, nitautumia kwa watoto kusomea na kuchaji simu, nashukuru sana”
Kwa upande wake, Fabian Ngailo mkazi wa kijiji cha Makewe amesema, “baada ya kupata umeme huu, najipanga kujenga nyumba kubwa na kuweka umeme pamoja na mashine ya kusaga”. Aidha, wameeleza kuwa kwa sasa hawatalala giza, na wataweza kununua TV na radio kwa kuwa sasa wana umeme kwenye nyumba zao.



