KENYA YAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KUHUSU WANAHARAKATI

{"data":{"pictureId":"a877e852da73424bb80c81efdb5d340a","appversion":"2.5.0","stickerId":"","filterId":"","infoStickerId":"","imageEffectId":"","playId":"","activityName":"","os":"android","product":"retouch","exportType":"image_export","editType":"image_edit"},"source_type":"vicut","tiktok_developers_3p_anchor_params":"{"source_type":"vicut","client_key":"aw889s25wozf8s7e","picture_template_id":""}"}
Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri nchini Kenya, Musalia Mudavadi, ameunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyotoa Mei 19, 2025, kuhusu wanaharakati kutoka nje kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania.
Akizungumza na kituo cha Televisheni cha Citizen, Mudavadi amesema kwamba kauli ya Rais Samia ina ukweli, na kwamba ingawa Kenya inaheshimu uhuru wa maoni, kuna wakati ambapo wanajamii wanakosa adabu na kuvuka mipaka.
“Sitaipinga (kauli ya Rais Samia) kwa sababu nadhani kuna ukweli ndani yake. Tuangalie hoja kadhaa: kiwango cha adabu, matusi tunayoyaona Kenya — pamoja na kuwa tuna uhuru wa maoni — kuna wakati kuna kuvuka mipaka,” amesisitiza Mudavadi wakati akijibu swali la mwandishi Yvonne Okwara, aliyemuuliza kama Serikali ya Kenya ina mpango wa kuchukua hatua za kidiplomasia kuhusu suala la ‘watovu wa adabu’.
“Rais Samia anasema watu wanavuka mipaka (katika kutoa maoni) Kenya — huo ni ukweli,” amesema Mudavadi. “Mimi ni Mkenya pia, ukweli ni kuwa namna tunavyofanya mambo na tunavyoongea, kwa sababu kuna uhuru wa maoni, hakuna heshima,” amesisitiza.
Wakati huo huo, Msemaji wa Serikali ya Kenya, Isaac Mwaura, amesema kuwa Tanzania ina haki ya kikatiba ya kujizuia kuingiliwa na watu kutoka nje, hasa iwapo inatambua kuwa mtu fulani hatakiwi kuingia nchini kwa sababu za usalama au mipango ya kitaifa.

Akijibu kuhusu hatua ya kuzuiwa kwa kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu, Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, na wanaharakati wengine wanne kuingia Tanzania, Mwaura amefafanua kuwa: “Ikiwa serikali ya mojawapo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaamua kumkataa mtu binafsi kuingia nchini mwao, ina mamlaka ya kufanya hivyo.”
Amesisitiza kuwa Serikali ya Kenya inaheshimu uhuru wa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na haiingilii maamuzi yao ya ndani.
“Ikiwa wameamua hivyo, huo ni uamuzi wao. Hatujui kwa nini wamemzuia mtu, na Serikali ya Kenya haihusiki,” amesema.
Ikumbukwe kuwa Mei 19, 2025, Rais Samia alionya kuhusu wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania — kauli iliyohusishwa na ujio wa wanaharakati kutoka Kenya waliokuja kufuatilia kesi ya Tundu Lissu.