WAWEKEZAJI WA OMAN WATUA TANZANIA – KUCHOCHEA MAPINDUZI YA SEKTA YA MAKAZI

0
1002091599

Tanzania imepiga hatua isiyosahaulika katika historia ya maendeleo yake baada ya kupata ziara ya kikosi cha wawekezaji wa ngazi ya juu kutoka Ufalme wa Oman, walioleta fursa kubwa za mabadiliko makubwa katika sekta ya makazi na maendeleo ya miji.

Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidha, na ulikuwa na malengo kadhaa ya kukuza mashirikiano ya kiuchumi mojawapo likiwa ni kuanzisha mabadiliko ya kimkakati yatakayochochea ukuaji wa sekta ya makazi kwa njia ya ubia wa kimataifa.

Katika kikao cha kihistoria kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) – Kambarage House, ujumbe wa Oman ulipokelewa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, pamoja na viongozi waandamizi wa taasisi hiyo.

Mazungumzo yalilenga kuibua fursa za uwekezaji katika miradi ya nyumba za gharama nafuu, miundombinu ya kisasa ya miji, na kuanzisha ushirikiano thabiti baina ya sekta binafsi na ya umma (PPP).

Sera ya Ubia ya NHC ya mwaka 2022 imekuwa nguzo muhimu inayovutia wawekezaji kama Oman kuwekeza katika miradi yenye tija kubwa kwa Watanzania. Miradi hii inalenga sio tu kujenga makazi ya bei nafuu, bali pia kuongeza ajira kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali za ujenzi, usimamizi wa miradi, na usambazaji wa vifaa vya ujenzi.

Balozi Saud Al Shidha alisisitiza kuwa ushirikiano huu unafungamanisha historia ndefu ya uhusiano wa kifamilia na kiutamaduni baina ya Oman na Tanzania, akiongeza kuwa zaidi ya Waomani 10,000 wenye asili ya Kitanzania wanaishi Oman.

“Uhusiano wetu si wa kibiashara tu, bali ni wa damu na historia. Tunalenga kuendeleza maendeleo endelevu kupitia miradi ya pamoja,” alisema Balozi Shidha.

Kwa upande wake, Hamad Abdallah alisema: “Huu si uwekezaji wa kawaida – ni mwanzo wa mapinduzi ya kimkakati katika sekta ya makazi nchini Tanzania. Watanzania wataona mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi.” Nikolay Anuashvili, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Uwekezaji ya Oman, aliongeza: “Tunajenga daraja la matumaini na ushirikiano wa kweli kati ya mataifa yetu.

Lengo letu ni kuleta makazi bora, miji bora, na maisha bora kwa Watanzania.”

Baada ya mazungumzo hayo ya kihistoria, pande zote mbili zilibadilishana zawadi kama ishara ya heshima na matumaini ya ushirikiano wa kudumu. Hii ni hatua ya wazi kuelekea kusaini makubaliano rasmi Juni mwaka huu, kutangaza zabuni Julai, na kuandaa ziara za wataalamu wa Oman Agosti 2025, kuimarisha utekelezaji wa miradi hii.

NHC inasisitiza kuwa ushirikiano huu ni fursa kwa Watanzania wote, hasa wajasiriamali wa sekta ya ujenzi, wasambazaji wa vifaa, wafanyabiashara wa ndani, na wananchi wanaotafuta makazi bora na ya gharama nafuu. Wote wanahimizwa kujiandikisha kwenye tovuti rasmi ya NHC ili kushiriki kikamilifu katika mabadiliko haya makubwa.

Kwa mshikamano wa kitaifa na ushirikiano wa kimataifa, Tanzania inaelekea kwenye enzi mpya ya maendeleo ya makazi, ikichochewa na dira thabiti ya NHC na wawekezaji wa Oman. Huu ni mwanzo wa mapinduzi ya kweli katika sekta ya makazi, na Watanzania wote wanatarajia mafanikio makubwa yanayokuja haraka

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *