WIZARA YA ARDHI YAHAMIA RASMI JENGO JIPYA MTUMBA

0
499539206_1463793561415882_7333933180632633453_n.heic

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza rasmi shughuli zake katika makao mapya yaliyopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo la kisasa lililojengwa na Mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hatua hiyo muhimu ya kihistoria iliongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, wakiongozana na watumishi wa wizara waliohamia rasmi katika jengo hilo jipya leo tarehe 19 Mei 2025.

“Leo hii sisi tumehamia rasmi na tuko tayari kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Wote wanaohitaji huduma zetu wanakaribishwa hapa Mtumba kwa sababu kuanzia sasa majukumu yote rasmi ya wizara yatatolewa kutoka katika jengo hili jipya,” alisema Mhe. Ndejembi kwa msisitizo, huku akihamasisha wananchi kujitokeza kwa ajili ya kupata huduma bila usumbufu.

Ujenzi wa jengo hilo umeleta taswira mpya ya ufanisi na ubora wa majengo ya serikali, likiwa ni miongoni mwa jitihada za kuimarisha miundombinu ya utendaji kazi wa taasisi za umma sambamba na azma ya serikali ya kuhamishia shughuli zake zote Dodoma.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa NHC, jengo hilo limetekelezwa kwa viwango vya kisasa na limezingatia mahitaji ya kiutendaji, mazingira rafiki kwa wateja, pamoja na mfumo bora wa TEHAMA kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.

Wananchi wengi wamepokea taarifa za kuhamia kwa wizara hiyo kwa furaha, wakieleza matumaini yao kuwa huduma zitakuwa karibu zaidi, bora zaidi, na kwa wakati, huku wakipongeza hatua hiyo kama sehemu ya utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *