WANANCHI NJOMBE WAOMBA WIGO WA MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME KATIKA VITONGOJI UONGEZWE


Wananchi wa vitongoji mbalimbali vya Mkoa wa Njombe wameiomba Serikali kuongeza wigo wa miradi ya kusambaza umeme ili iweze kutekelezwa katika vitongoji vyote.
Wakizungumza katika nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara inayoendelea wakati wa kampeni ya kutoa elimu na kuhamasisha umma kuunganisha umeme katika Mkoa wa Njombe, wananchi hao wameiomba Serikali kuongeza wigo wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na taasisi nyingi zilizopo katika maeneo yao.

Mikutano hiyo imefanyika katika vijiji vya Ibatu, Usetule, Manga, Kifumbe, Mtulingala, Mbugani na Nyamande, ambapo wananchi wa vitongoji vya Magomati, Mjimwema, Kidete, Mtanga, Ilongo, Kisaula, Matangini, Mvengi B na Nyamande A, wameiomba Serikali kuongeza miradi ya kusambaza umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa.
Aloyce Ng’angalila mkazi wa Kitongoji cha Magomati Kijiji Cha Usetule amesema, “nyumba zilizopitiwa na nguzo za umeme ni chache na ambazo hazijapitiwa na mradi huo wa umeme ni nyingi, naomba REA itusaidie kupata Umeme katika maeneo yaliyobaki”.

Wakiongea katika mkutano uliofanyika katika Kijiji Cha Mtulingala, Christina Mdendemi na Anet Mtenga wamesema kuwa hawajaunganishiwa umeme katika biashara na makazi yao hivyo wanatumia nishati ya umeme jua ambayo haikidhi mahitaji yao na kusababisha wafunge biashara mapema. Hivyo wameiomba Serikali kuongeza nguzo katika maeneo yao ili waweze kuunganisha umeme.
Nae, Mwenyekiti wa Kijiji Cha Ibatu amesema kuwa nyumba zaidi ya 30 hazijafikiwa na nguzo za umeme ikiwemo Ofisi ya Kijiji, hivyo anaomba Serikali kupeleka umeme katika taasisi hiyo na maeneo mengine ambayo hayajafikiwa.

Akijibu hoja za wananchi hao, Meneja wa REA Mkoa wa Njombe, Mha. Marlon Bulugu ameeleza kuwa Serikali imeandaa mpango wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote kwa kipindi cha miaka mitano na kuwa utekelezaji wake unafanyika kwa awamu.
Aidha, aliwataka wananchi ambao majengo yao yapo katika wigo Mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji (HEP 2A), ambao utekelezaji umeanza kuandaa majengo yao kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kwa kufanya wiring na pia kutumia umeme kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
