UWEKEZAJI MAHIRI KUINGIZIA SERIKALI BILIONI 3.3 KWA MWAKA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA inatarajia kupata Shilingi Bilioni 3.3 kwa mwaka kutoka kwenye Mkataba wa Uwekezaji Mahiri kwenye maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas- SWICA) kwa kitalu cha uwindaji katika Pori la Akiba Selous.
Mhe. Chana ameyasema hayo leo 19 Mei,2025, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Sambamba na hilo, Mhe. Chana amesema Serikali imeendelea kurejesha stahili kwa wanufaika wa shughuli za uhifadhi na utalii ambapo jumla ya Bilioni 17.1 zimetolewa kwa wanufaika. Aidha, TAWA imechangia jumla ya shilingi za kitanzania Milioni 162 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na jamii ikiwemo mradi wa kuchimba kisima katika Wilaya ya Rufiji, Ununuzi wa madawati 595 katika Wilaya za Bariadi, Itilima na Longido, Ununuzi wa viti na meza kwa zahanati ya Visakazi iliyopo Wilaya ya Chalinze pamoja na ununuzi wa mifuko ya saruji 325 kwa ajili ya kuchangia miradi ya ujenzi katika Wilaya za Makete, Wanging’ombe, Mbarali, Sumbawanga, Chemba na Nanyumbu.

Katika kuhakikisha hifadhi zilizoko chini ya TAWA zinakuwa na miundombinu bora kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na shughuli za utalii, Mhe. Chana amesema TAWA imekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 120.5, katika Pori la Akiba Pande (km 10.5), Rungwa (km 80) na Makuyuni (km 30). Pia, ujenzi wa barabara unaendelea katika Mapori ya Akiba Wami-Mbiki na Mpanga-Kipengere. Aidha, Mamlaka imekamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya Askari katika Pori Tengefu Lunda Nkwambi na Mapori ya Akiba na Lwafi na Wamimbiki.
Kadhalika, Mhe. Chana amesema TAWA imendelea kutatua migogoro ya mipaka katika maeneo ya hifadhi kwa kuweka alama za mipaka na jumla ya vigingi 691 vimesimikwa katika Pori la Akiba Kilombero na uhakiki wa mipaka ya Mapori ya Akiba ya Selous na Swagaswaga umekamilika.

Vilevile, Mhe. Chana ameongeza kuwa TAWA imeendelea kutangaza shughuli za utalii kupitia maonesho mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa na kufuatia juhudi hizo idadi ya watalii waliotembelea maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka kwa ajili ya shughuli za utalii kwa mwaka 2024-2025, imeongezeka kwa asilimia 35.1% kwa watalii wa picha na idadi ya wawindaji wa kitalii wameongezeka kwa asilimia 9.5% kulinganisha na mwaka 2023-2024

.