KILINKI YA SHERIA BILA MALIPO YAZINDULIWA SINGIDA


Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida imezindua rasmi Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida. Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani Manispaa ya Singida.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Singida na kuja kuzindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kuwa ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo kutatuliwa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.

Mhe. Dendego amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati hiyo pamoja na masuala mengine, kutasaidia Kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, kuwawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria katika maeneo yao, Kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushirikiana na wadau wengine katika kutatua kero za wananchi na kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi.
“Naomba kukuahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa nitazisimamia Kamati hizi kikamilifu ili ziweze kuwa na tija katika mkoa wetu.” Amesema Mhe. Dendego

Katia hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Singida ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Sheria bila malipo ili waweze kupata huduma mbalimbali za kisheria hususani katika masuala ya mirathi, Ardhi, ndoa na Ajira.
kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida ni mojawapo ya hatua za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.

“Lengo kuu la uanzishwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya ni kurahisisha usimamizi wa utoaji wa ushauri wa kisheria kwa wananchi katika maeneo husika”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria kwa Mkoa wa Singida utafuatiwa na Kliniki ya sheria kuanzia tarehe 19 hadi 25 Mei, 2025 ambapo huduma za ushauri wa kisheria zitatolewa kwa wananchi bila malipo, ambapo amesisitiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itatoa huduma hizo kwa ubora.
“Tunawaahidi tutatoa huduma hii bila malipo kwa wananchi na kwa weledi mkubwa”.* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Kliniki ya Sheria Bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida imezinduliwa tarehe 19 Mei na itaendelea kutoa huduma za kisheria kwa Wanachi wa Mkoa wa Singida hadi tarehe 25 Mei, 2025 katika Viwanja vya Stendi ya zamani Mansipaa ya Singida.