BUNGE LAIDHINISHA BAJETI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII BILIONI 359.9

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Shilingi bilioni 359.98 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele 10 huku Shilingi bilioni 105.74 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Tulia Ackson alisema hayo leo Mei 19,2025 jijini Dodoma huku akisisitiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuitumia bajeti hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) akihitimisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 alisema kuwa Serikali inatarajia kufanya mabadiliko yatakayoruhusu mashirika mawili kukukusanya mapato na kutumia fedha (rentetion).
Mashirika hayo ni Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) ambayo kuanzia mwaka 2020 makusanyo ya mapato yalikuwa yanaenda Mfuko Mkuu wa Serikali na baadaye kurejeshwa.
Dkt. Chana amesema lazima kuwe na rentetion kwa kuwa katika maeneo ya utalii yanahitaji marekebisho mbalimbali ikiwemo madaraja.

“Kutakuwa retention kwa mashirika yetu haya ya TANAPA na NCCA na baadaye tunavyooendelea tutaangalia jinsi tunavyoweza kuwa na retention kwa mashirika mengine,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu makadirio hayo alielezea changamoto hiyo ya mashirika hayo kutobakia na makusanyo yake kama ilivyokuwa awali.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, TANAPA na NCAA yamepata changamoto ya kujiendesha katika maeneo ya kutolea huduma kwa watalii na kushindwa kufanya shughuli za uhifadhi kwa ufanisi.
“Hali hii inachangia watalii wengi nchini kushindwa kufika katika vivutio vingi kwa wakati.Kamati inaitaka Serikali kurejesha utaratibu wa TANAPA na NCAA kukusanya na kutumia ili kuwezesha taaasisi hizi kujiendesha kwa ufanisi,”amesema.