SERIKALI YAKABIDHI SHILINGI BILIONI 2.25 KWA WANUFAIKA WA SHUGHULI ZA UTALII

0
IMG-20250517-WA0047

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekabidhi gawio la shilingi za kitanzania Bilioni 2.25 kwa wanufaika 51 wa shughuli za uhifadhi na utalii zikiwemo Halmashauri za Wilaya 25 (Milioni 368), Vijiji 20 (Milioni 385) na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) 6 (Bilioni 1.5).

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi hizo, leo 17 Mei, 2025, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana (Mb) amesema Serikali imeweka miongozo ya kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za utalii na kuyarudisha kwa wanufaika ikiwemo Vijiji, WMA na Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na kuongeza chachu kwa wananchi katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.

“Utoaji wa fedha hizi kunalenga kuongeza chachu kwa jamii katika kuimarisha usimamizi wa Rasilimali ya Wanyamapori, kukuza utalii na kuongeza mapato katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA” amesema Mhe. Chana.

Aidha, Mhe. Chana amewasisitiza wanufaika wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii kuhakikisha kwamba wanaweka mipango thabiti ya matumizi ya fedha hizo ikiwemo kuboresha uhifadhi na kuimarisha miradi ya maendeleo ya jamii.

Sambamba na hilo, Mhe. Chana amewapongeza wadau waliopewa gawio kwa jitihada wanazozichukua katika uhifadhi wa wanyamapori na kukuza utalii unaopelekea kuongezeka kwa kipato kwa wananchi na kuimarisha maendeleo kwa jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mlage Kabange amesema Fedha zinazotolewa kama gawio kwa wanufaika zinaleta matokeo chanya katika kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori, kulipa mishahara ya watumishi walioajiriwa kwenye WMA hususan Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS), kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii katika maeneo yao.

Naye, Mhe. Robert Marunya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, kwa niaba Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Serengeti, Babati, Monduli na Ngorongoro ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa gawio hilo na amesema kuwa fedha hizi zitaenda kuongeza pato la Halmashauri pamoja na kushughulikia masuala ya uhifadhi ikiwemo kupunguza migogoro ya wanyamapori na binadamu.

Vilevile, Kwa niaba ya Wenyeviti wa Jumuiya za Hifadhi za wanyamapori (WMA), Bw. Elias Chama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ikona WMA amesema wanashukuru ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAWA, Aidha ameongeza kuwa katika hifadhi yao ya Ikona fedha hizi zitaenda kufanya kazi kusudiwa ambayo ni uhifadhi na utalii.

Hafla hii imehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Naibu Katibu Mkuu (Maliasili), CP. Benedict Wakulyamba, Naibu Katibu Mkuu (Utalii), Nkoba Mabula, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dr. Alexander Lobora pamoja na Wakurugenzi wengine kutoka Idara mbalimbali zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *