RAIS WA FINLAND ATEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA

0
IMG-20250515-WA0071

Rais wa Jamhuri ya Finland, Mhe. Alexander Stubb, ametembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania jijini Dar es Salaam na kuonesha kufurahishwa na maonesho ya historia ya mwanadamu yaliyopo katika jumba hilo la kihistoria.

Akizungumza katika ziara hiyo leo, Mei 15, 2025, Rais Stubb amesema kuwa amepata fursa ya kujionea historia ya mwanadamu, jambo lililomgusa sana na kumpa uelewa wa kina kuhusu asili ya binadamu.

“Nimejionea historia ya mwanadamu, sasa najua tulikotoka,” alisema Rais Stubb huku akisisitiza kuwa mashirikiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Finland yalianza tangu nchi hizo zilipopata uhuru—Finland mwaka 1917 na Tanzania miaka ya 1960,”amesema.

Ameongeza kuwa uhusiano huo wa kihistoria ulianza tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na Rais wa kwanza wa Finland.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa ujio wa Rais Stubb ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rais Stubb ameona fuvu la Zinjanthropus, zana za jadi, na hatua mbalimbali za maendeleo ya mwanadamu. Hili ni jambo la heshima kubwa kwa taifa letu,” amesema Mhe. Chana.

Aidha, ameeleza kuwa kupitia ziara hiyo, Tanzania na Finland zimekubaliana kuendeleza mashirikiano katika maeneo ya mafunzo, tafiti za pamoja, na kubadilishana uzoefu katika sekta ya makumbusho na malikale.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Noel Luoga, amesema kuwa ziara hiyo imekuwa chachu na hamasa kubwa kwa taasisi hiyo kuendelea kutangaza utalii wa malikale.

“Tunatarajia kushirikiana na Finland katika tafiti, kuboresha maonesho kwa kutumia teknolojia za kisasa, pamoja na kuhakikisha makumbusho yanafika kwa jamii,” amesema Luoga.

Ziara hiyo pia imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na watendaji wa baadhi ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *