TANZANIA NA ETHIOPIA, NCHI PEKEE AFRIKA ZENYE KUFANYA KAZI NA SERIKALI YA FINLAND- RAIS SAMIA

Tanzania na Ethiopia ndiyo nchi pekee kutoka barani Afrika zenye kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na nchi ya Finland kwa zaidi ya miaka 60 sasa, suala ambalo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa jambo lenye Heshima na lenye manufaa makubwa kwa wananchi wa pande hizo zenye kuhusiana kibiashara na kidiplomasia.
Kauli ya Rais Samia imekuja kufuatia mazungumzo yake na Rais wa Finland Mhe. Alexander Stubb, ambaye amewasili nchini Tanzania leo Mei 14, 2025 kwa ziara ya Kikazi kufuatia mualiko wa Rais Samia, wakisherehekea miaka 60 ya ushirikiano huo uliojengwa katika misingi ya urafiki, maelewano na kuheshimiana miongoni mwao.
“Wakati wa mazungumzo yetu Rais Alexander Stubb ametuambia kuwa Finland inafanya kazi na nchi mbili tu ndani ya Afrika, nayo ni Ethiopia na sisi Tanzania. Hii ni heshima kubwa kwetu, tunawashukuru sana. ” Rais Samia amemueleza Rais stubb mbele ya wanahabari baada ya mazungumzo yao ya faragha Ikulu ya Magogoni Jijini Dar Es salaam.
Katika maelezo yake, Rais Samia amebainisha kuwa wamejadili na kukubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta zinazogusa maisha ya watanzania na watu wa Finland ikiwemo uchumi wa buluu, nishati, elimu na teknolojia, akiwakaribisha pia wafanyabiashara alioambatana nao kuangalia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
Kwa upande wake Rais Stubb kando ya kuonesha dhamira yake ya kuendeleza mahusiano na Tanzania, akieleza kuwa anaiangalia Tanzania kama mshirika wa karibu, akiahidi kuendeleza mahusiano hayo kwa maslahi ya raia wa pande zote na wakiamini katika usawa, ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na Tanzania imekuwa na sehemu kubwa kwenye mioyo ya raia wa Finland.
“Mimi binafsi, nikiwa natoka nchi ndogo kaskazini mwa Ulaya yenye watu milioni 5.6, naiangalia Tanzania kama mshirika wa karibu sana, sasa na hata siku zijazo. Na huwezi jua, huenda tukawa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa pamoja, ifikapo mwaka 2029 au 2030.”, amesema Rais Stubb.
Rais huyo ambaye aliwahi kuja Tanzania miaka 22 iliyopita, akiwa Waziri wa Biashara, amesema wamezungumzia pia suala la amani ya kikanda, mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijinsia na maeneo mengine ya ushirikiano.
“Katika mazungumzo yetu tulikubaliana kwamba malengo yetu si tu kuwa na uhusiano mzuri, bali kufanya kazi pamoja kudumisha sheria za kimataifa. Lengo letu ni jambo hilo kuakisi Afrika nzima,” amesema Rais Stubb.