CCM DAR WAIPA KONGOLE DAWASA KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA MAJI

0
IMG-20250512-WA0024

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abbas Mtemvu ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa jitihada kubwa za kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati ukiwemo mradi wa maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo).

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa kutembelea  miradi ya maendeleo na kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji wa Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo)uliokamilika na unategemea kunufaisha wakazi zaidi ya 450,000 wa Wilaya za Ubungo, Segerea, Ukonga, Kisarawe na Temeke

Amesema kuwa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi za kutekeleza miradi ya kimkakati ya majisafi kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

“Niwapongeze DAWASA kwa kuweza kuweka mikakati madhubuti ya kujenga miradi na kusambaza maji kwenye maeneo ya Wananchi kwa lengo la kuonesha thamani ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan,” amesema Mhe. Mtemvu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Albert Msando ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa jitihada kubwa za kuboresha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ubungo hali inayosaidia kupunguza malalamiko na kutoa muda wa kufanya Wananchi kufanya shughuli za maendeleo.

Amemshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele Wilaya ya Ubungo kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya kunufaisha wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa  Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Modesta Mushi amesema kuwa mradi wa maji Bangulo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 36.9 ni mradi wa mfano ambao unanufaisha wakazi wa Wilaya za Ubungo, Segerea, Ukonga, Kisarawe na Temeke

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi umehusisha ujenzi wa tenki la Maji lita milioni 9, kituo cha kusukuma maji cha uwezo wa lita 500,000 pamoja na ufungaji wa pampu 3 eneo la Kibamba zenye uwezo wa kusukuma maji lita 590,000 kwa saa.

Ameongeza kuwa mradi huu utawanufaisha Wananchi wa Ubungo katika kata za King’azi, Saranga, Msigani na Kwembe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *