NAIBU WAZIRI SANGU ATANGAZA MUUNDO MPYA WA UTUMISHI WA KADA YA UUGUZI NA UKUNGA

0
IMG-20250510-WA0008

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu ametangaza kuanza kutumika kwa Muundo mpya wa Utumishi wa Maendeleo ya kada za Uuguzi na Ukunga ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Amesema utekelezaji wa muundo huo utasaidia kuongeza morali ya utendaji kazi kwa wataalamu wa Kada hiyo pamoja na kuboresha maslahi yao.

Amesema Serikali imesikia kilio cha Wauguzi hao kilichodumu kwa zaidi ya miaka 12 kutokana na muundo wa mwaka 2009 ambao unatumika hadi hivi sasa kuwa changamoto nyingi ikiwemo kutokutambua kada ya Wauguzi na Wakunga wenye shahada ya juu na wenye shahada ya uzamili.

Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo Mkoani Iringa wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama Cha Wauguzi Tanzania unaofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo kukiwa na jumla ya Washiriki 1500.

Amesema kutokana na changamoto za muundo huo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais. UTUMISHI na Utawala Bora , Baraza la Uuguzi na Ukunga na Vyama vya Kitaaluma ilipitia muundo huo na kurekebisha changamoto zilizokuwepo na hivi sasa upo tayari kwa hatua za utekelezaji.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeamua kurekebisha muundo huo kwani muundo huo umekuwa na mapungufu kwa wataalamu wa kada hiyo.

Katika hatua nyingine Mhe.Sangu ameziagiza Mamlaka za ajira nchini ifikapo Mei 31, 2025 zihakikishe zinawasilisha orodha ya Watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo wakiwemo wauguzi na wakunga huku akisisitiza kuwa bajeti ya kiasi cha Sh. Bil.207 zimeshatengwa kwa ajili ya upandishaji vyeo

Wakati huo huo, Mhe.Sangu amezitaka Mamlaka za Ajira nchini kuhakikisha orodha ya Watumishi wakiwemo Wauguzi wanaodai malimbikizo ya mishahara yawasilishwe Ofisi ya Rais Utumishi ifikapo Mei 31, 2025 yakiwa yamehakikiwa, ili baada Ofisi hiyo kujiridhisha yawasilishwe Hazina kwa ajili ya taratibu za malipo

Akizungumzia suala la uhaba wa Watumishi wa Kada hiyo ya Wauguzi, Mhe.Sangu amesema Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha Uongozi amewekeza vya kutosha kwenye sekta ya afya ikiwemo vifaa tiba na miundombinu ya afya.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu amesema Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa kibali cha ajira zipatazo 33, 212 na kati ya hizo takribani ajira 11,000 ni kwa ajili ya kada ya afya ikiwemo wauguzi na wakunga hali itakayochangia kuongeza nguvu na ufanisi kwa Watumishi wa kada hiyo katika utoaji huduma bora kwa wananchi

Awali, Rais wa Chama cha Wauguzi, Bw. Alexander Baluhya amesema uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye sekta ya afya lakini umekuwa hauendani na huduma zinazotolewa kutokana na uhaba wa Wauguzi na hivyo kupelekea wananchi kupata huduma zisizoridhisha.

Amesema hapo awali kulikuwa na vituo vichache vya afya lakini kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan idadi ya vituo hivyo imeongezeka maradufu hadi kufikia vituo vipatavyo 1,038 na hivyo kupelekea Wauguzi na Wakunga kuwa na majukumu mengi kupita uwezo wao.

Bw.Baluhya amesema suala la upandishaji madaraja kwa Wauguzi imekuwa changamoto kubwa licha ya Wauguzi hao kuwa sifa stahiki za kuweza kupanda vyeo.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri na kushusha morali kwa Wauguzi hao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Peter Serukamba amewataka Wauguzi hao kufanya kazi kwa weledi huku akiwasisitiza umuhimu wa kujiendeleza ili kujitafutia maarifa mapya kutokana na mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayotokea duniani kote.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejenga vituo vya Afya na Zahanati kila kona ya nchi hivyo hilo haliwezi kutimia kama Wauguzi watakuwa hawana maarifa mapya pamoja na kuwa na lugha mbaya pindi wanapowahudumia wagonjwa.

Hata hivyo Mhe.Serukamba ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri za Wilaya nchini kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha Wauguzi wanapandishwa madaraja yao pamoja na kulipwa stahiki zao pindi wanapokwenda likizo.” Tusiwabebeshe mzigo w Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora haya mengine yapo chini ya uwezo wa Halmashauri zetu ” amesisitiza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *