DKT. TULIA AZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME KATIKA VITONGOJI 105 MKOA WA MBEYA


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson leo Mei 10, 2025 amezindua rasmi mradi wa kusambaza umeme katika Vitongoji 105 katika Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kumkabidhi rasmi Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye ni Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu, Usafirishaji na Usambazi Umeme (ETDCO), Mhe. Dkt. Tulia amewasisitiza wananchi waliopo maeneo ambapo mradi utapita waanze kufanya maandalizi ya kupokea umeme katika nyumba zao.

“Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuonyesha mapenzi makubwa kwa Watanzania na hasa wananchi wa Mbeya. Fedha hizi zitakazotekeleza mradi huu zingeweza kupelekwa katika miradi mingine. Niwasisitize wananchi ambao mradi huu utapita muanze kuandaa nyumba zenu mapema kwa ajili ya kupokea umeme na kuingiza katika nyumba zenu pindi mradi utakapowafikia.
Na hii ndio njia pekee ya kumuonyesha Mhe. Rais kwamba alifanya maamuzi sahihi ya kutoa fedha hizo kwa ajili ya kufikishiwa umeme kwenye vitongoji vyetu,” amesema Mhe. Dkt. Tulia huku akimsisitiza mkandarasi huyo kuhakikisha anamaliza mradi huo ndani ya muda uliopangwa.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amewasisitiza wananchi kutunza miundombinu hiyo ya umeme kwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi hao wa vijijini nao wanapata huduma ya umeme kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa mradi huo uliolenga kusambaza umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo unagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 10.9.
“Mkoa wa Mbeya una jumla ya Vijiji 533 na vijiji vyote tayari tumevifikishia umeme. Na sasa tunaendelea na safari ya kupeleka umeme katika vitongoji ikiwa na dhamira ya Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya umeme,” amesema Mhandisi Olotu.
