DKT. MWIGULU AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA YA FEDHA KUZINGATIA MISINGI YA KAZI NA UTAWALA BORA

0
IMG-20250510-WA0034

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewataka Watumishi wa Wizara ya Fedha, kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia misingi ya kazi na utawala bora ili kuepusha malalamiko yasiyo na lazima kutoka kwa wadau wake wakiwemo wananchi.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha, lililofanyika katika katika Kituo cha Mikutano cha APC, kilichoko Bunju mkoani Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba aliutaka Uongozi wa Wizara kumchukulia hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu mtumishi yeyote atakayebainika na kuthibitika kwenda kinyume na misingi ya maadili katika utendaji kazi ili kulinda heshima ya Wizara.

‘’Ninatambua kwamba mnafahamu misingi ya utendaji kazi katika utumishi wa umma, hivyo, si jambo jema kusikia mtumishi yeyote wa Wizara ya Fedha anakiuka misingi ya utawala bora katika utumishi wa umma’’, alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Pia, Mhe. Dkt. Nchemba aliwapongeza watumishi wote wa Wizara hiyo kwa kazi na mchango wao moubwa uliofanikisha majukumu yake ya kuismamia uchimi wa nchi na kuwezesha upatikanaji wa Fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Aliwataka Watumishi wa Wizara kuendelea kufanyakazi kwa ushirikiano kati ya Watumishi ndani ya Idara, Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, na kuzielekeza Taasisi kutekeleza majukumu yao ya msingi kama inavyoratajiwa na Serikali pamoja na wadau wengine.

Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa kutokana na Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Wizara katika kuwapatia mafunzo Watumishi wake, hivyo ni lazima matokeo ya mafunzo hayo yaonekane kwa vitendo kupitia utendaji wa kila mtumishi, na kusisitiza umuhimu wa Watumishi kuendelea kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo la Watanyakazi ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa lengo kuu la Baraza la Wafanyakazi ni kuwashirikisha Wafanyakazi katika utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa kushirikiana na Uongozi ikiwa ni pamoja na kuishauri Wizara juu ya ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili huduma zinazotolewa na Wizara zikidhi matarajo ya wateja.

Dkt. Mwamba aliongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wizara imepata mafanikio mbalimbali yakiwezo kupandishwa vyeo kwa Watumishi 484 wa kada mbalimbali na kulipa jumla ya shilingi 521,980,765/= yakiwa ni malimbikizo ya mishahara kwa Watumishi wa Wizara.

‘’ Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imeshatoa kibali ili watumishi wenye sifa waweze kupandishwa vyeo. Uchambuzi wa awali umebaini kwamba watumishi 313 wana sifa za kupandishwa vyeo’’ alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba aliongeza kuwa Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi ni mwendelezo wa mikutano mingine ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka ambapo kupitia mikutano hiyo wajumbe wamekuwa wakitoa maoni na mapendekezo ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maslahi ya watumishi na utendaji kazi wa Wizara.

Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha, umekutanisha Wajumbe kutoka Makao Makuu ya Wizara, Wakuu wa Hazina Ndogo na Wahakikimali kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *