NHC YASHIRIKI MAONYESHO MAALUM YA SEKTA YA MAENDELEO YA MILKI KWA WANADIASPORA NCHINI UINGEREZA

0
495047471_698297619554981_6540421191332840741_n.heic

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, limefanikiwa kushiriki Maonyesho Maalum ya Sekta ya Maendeleo ya Milki kwa Wanadiaspora yaliyofanyika katika hoteli ya kifahari ya London Marriott Hotel Grosvenor mnamo tarehe 3 Mei 2025, kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 5 usiku.

Maonyesho haya yalilenga kuwaelimisha na kuwahamasisha Watanzania wanaoishi Uingereza kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya milki nchini Tanzania, huku Shirika la Nyumba la Taifa likitoa maelezo ya kina juu ya miradi yake ya kimkakati ya ujenzi wa nyumba za kisasa na za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mgeni rasmi katika tukio hili alikuwa Mheshimiwa Balozi Mbelwa Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambaye aliwasisitiza Watanzania waishio nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji nyumbani, hususan katika sekta ya ujenzi na maendeleo ya makazi. Balozi Kairuki alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa juhudi zake za kuwafikia Watanzania wanaoishi nje ya nchi na kutoa huduma zenye uwazi, uhakika na weledi.

Watanzania Wanadiaspora walijitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho haya, ambapo walipata nafasi ya kuuliza maswali, kupata ushauri wa kitaalamu, na kujiandikisha kwa ajili ya miradi ya nyumba inayotekelezwa na NHC. Ushiriki wao mkubwa ni ishara ya dhamira ya kweli ya kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa.

Shirika la Nyumba la Taifa litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Watanzania wanaoishi nje ya nchi, katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata nafasi ya kumiliki nyumba bora na salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *