KUMILIKI KADI YA MPIGA KURA ZAIDI YA MOJA NI KOSA KISHERIA – KAILIMA

Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura anastahili kujiandikisha mara moja na kupewa kitambulisho kimoja cha mpiga kura.
Kailima amefafanua kuwa, ikiwa kadi ya mpiga kura imeharibika kwa namna yoyote hali inayopelekea kutokutumika kwenye zoezi la upigaji kura basi mwananchi atalazimika kufika katika kituo cha eneo lake kuboresha taarifa zake ikiwa ni pamoja na kubadili kadi yake na sio kuchukua kadi nyingine.


Kailima amezungumza hayo leo Mei 3, 2025 alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Cg Fm Radio mjini Tabora, akisisitiza kuwa,
ni kosa kisheria kwa mwananchi kumiliki kadi ya mpiga kura zaidi ya moja.
Mkurugenzi huyo yupo katika ziara ya kutembelea vituo mbalimbali vya kuhakiki na kuboresha taarifa za mpiga kura katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili lililoanzia nchini Mei 1, 2025.