WADAU WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA KATIKA ZAO LA MPUNGA

0
IMG-20250502-WA0002

Wadau wa zao la mpunga nchini wametakiwa kuzichangamkia fursa zinazopatikana kwenye mnyororo mzima wa thamani ya zao hilo ambalo ni la pili kwa kukua kwa kasi nchini, huku uzalishaji wake umeongezeka kwa asilimia 5 kutoka mwaka 2010.

Amesema hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar wakati akifunga Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Zao la Mpunga kwa niaba ya Katibu Mkuu Gerald Mweli, uliofanyika tarehe 24 Aprili 2025, katika Hoteli ya St. Gasper, jijini Dodoma.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ilikuwa “Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na matokeo chanya ya Tasnia ya Mpunga”.

Wakati wa hotuba yake, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar ameeleza kuwa tija ya zao hilo inatarajiwa kuongezeka kutoka tani 2 kwa hekta hadi kufikia tani 4.4 kwa hekta katika kilimo cha mvua na tani 7.34 kwa hekta katika kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupandisha bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi Bilioni 294.16 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.249 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo ongezeko hilo la bajeti ya Wizara inachangia kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa zao la mpunga.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira ameshauri wakulima wa zao la mpunga kutumia kilimo cha umwagiliaji na mbegu bora zenye kuhimili mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza zaidi tija na uzalishaji.

Aidha, Mwakilishi wa Kampuni ya Japan International Cooperation Agency (JICA) Tanzania, Bw. Ara Hitoshi amesema ushindani kwenye uzalishaji wa zao la mpunga unaongezeka na utasaidia kufanikisha azima ya Serikali ya kukuza zaidi kilimo cha zao la mpunga.

Washiriki waliohudhuria ni pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Wizara ya Viwanda na Biashara; Makatibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa mikoa ya Mbeya, Shinyanga, Katavi, Tabora na Morogoro; Wasindikaji na Wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *