REA YAENDELEA NA UHAMASISHAJI MATUMIZI BORA YA NISHATI YA UMEME NA UUNGANISHAJI WATEJA, KILIMANJARO

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya umeme kwa Watanzania ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi bora ya nishati, kuhamasisha kuunganisha umeme, tahadhari za umeme pamoja na utunzaji wa miundombinu ya umeme.
Hayo yamebainishwa na Wataalam wa REA waliofika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutumia fursa ya miradi ya REA inayotekelezwa mkoani Kilimanjaro.


Akizungumza katika mkutano na wananchi, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Abdulrazack Mkomi amesema kuwa, lengo na dhamira ya serikali ni kuona mabadiliko yanatokea katika maeneo ya vijijini hasa kwenye nyanja za kiuchumi, afya, elimu na huduma zote muhimu za kijamii kwa ujumla.
Katika kunifanikisha hilo serikali kupitia wakala wa Nishati vijijini umeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini ikiwemo usambazaji wa nishati ya umeme ili nishati hiyo itumike kama silaha ya kuleta mabadiliko Vijijini.


Ameongeza kuwa, ili kuhamasisha matumizi bora ya nishati ya umeme, REA itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa kupita kaya kwa kaya , kitongoji kwa kitongoji , kijiji kwa kijiji ili kila mwanachi aweze kutumia nishati ya umeme vizuri na kujiletea maendeleo.
Naye, Mhandisi wa Miradi ya REA mkoa wa Kilimanjaro, Kelvin Melchiad amesema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kuwahamasisha wananchi kuunganisha umeme kwenye vitongoji baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme kwenye vijiji vyote nchini.

Mha. Kelvin ameongeza kuwa, Serikali imeweka mkazo katika kusambaza umeme kwa watanzania ili kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kujenga uchumi imara na kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kwa watanzania wote.
“Kufikisha miundombinu ya umeme hadi kwenye vitongoji kumekuwa kipaumbele muhimu katika juhudi za kuboresha uchumi na maisha ya Watanzania. Kupitia uunganishaji umeme, kutachochea ongezeko la viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuboresha huduma za afya na elimu,” amesema Mha. Kelvin.