BUNGE LAMPONGEZA DKT. MWAPINGA KWA KUIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA

0
InShot_20250429_230301914

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa niaba ya Bunge la Tanzania, ametoa salamu za pongezi kwa Dkt. Deo Mwapinga kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR).

Uchaguzi huo ulifanyika tarehe 25 Aprili 2025 katika Jiji la Luanda, nchini Angola, wakati wa Mkutano wa Wabunge kutoka Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu waliokutana kujadili masuala ya amani, usalama na utawala wa kidemokrasia, sambamba na kupitisha maamuzi muhimu kuhusu uongozi wa FP-ICGLR.

Jukwaa hilo linajumuisha Mabunge kutoka nchi 12 wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu, likiwa na dhamira ya kusaidia utekelezaji wa Itifaki ya mwaka 2006 kuhusu kuimarisha amani, usalama, demokrasia, utawala bora na haki za binadamu katika ukanda huo.

Katika nafasi yake mpya ya Katibu Mkuu, Dkt. Mwapinga atakuwa na jukumu la kuratibu shughuli na programu mbalimbali za Jukwaa hilo, likiwa na makao makuu yake mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Majukumu haya yanajumuisha pia kuimarisha mazungumzo ya Mabunge ya nchi wanachama na kuhamasisha mshikamano katika kufanikisha malengo muhimu ya maendeleo ya kikanda.

Akitoa pongezi hizo Bungeni, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesemaa, ni heshima kubwa kwa Tanzania kupata nafasi ambayo kimsingi nimatokeo ya diplomasia imara inayofanywa na Rais wetu wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukanda wa afrika na duniani kwa ujumla kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kubaki kwenye ramani na kuwa na ushawishi mkubwa.

Mhe. Spika amesema, Kikosi cha Tanzania kilichoenda Luanda, Angola kuhakikisha Tanzania inapata ushindi huu kiliongozwa na Naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu pamoja na wabunge ambao ni Mhe. Elibariki Kingu na Mhe. Eng. Ezra Chilewesa.

Sambamba na salamu hizo, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kutangaza kwa jamii mafanikio ya Watanzania wanaoshika nafasi kubwa na za kimkakati duniani, ili kuonesha thamani na uwezo mkubwa wa rasilimali watu wa Tanzania katika nyanja za kimataifa.

Bunge la Tanzania linaungana na Watanzania wote kumpongeza Dkt. Deo Mwapinga kwa mafanikio haya makubwa yanayochochea hadhi ya Taifa letu katika medani ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *